1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walibnan wamsubiri kwa shangwe na furaha Papa Benedikt wa 16

14 Septemba 2012

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, Benedikt wa 16, ameondoka Vatikani kuelekea Libanon ambako anatarajiwa kuwatolea mwito wakristo milioni 15 wa Mashariki ya kati waishi kwa amani pamoja na waislamu .

KIongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Benedikt wa 16Picha: dapd

Akiongoza ujumbe mkubwa wa makadinali kadhaa, Papa Benedikt wa 16 anatarajiwa kuwasili wakati wowote kutoka sasa  mjini Beirut.

Ziara hii inasadif miaka 15 baada ya ile ziara ya kihistoria iliyofanywa na mtangulizi wake,Johanna Paulo wa Pili, aliyeitaja kuwa ni "Risala",nchi hiyo ya mchanganyiko wa waumini wa dini tofauti na ambao wanatofautiana tangu katika suala la siasa ya ndani mpaka kuhusiana na vita nchini Syria.

Pirikapirika za kumkaribisha kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni zimeshika kasi, huku hatua za usalama zikiimarishwa mjini Beirut tangu angani mpaka ardhini.

Kanisa kuu la St. George mjini Beirut LibanonPicha: DW/D.Hodali

Jamii zote za wakaazi wa Libanon,wakristo tangu wakatoliki mpaka waorthodox,waislam tangu wa sunni mpaka wa shiya na wadruz wamejiandaa kumkaribisha Papa Benedikt wa 16.

"Libanon inasubiri ziara ya amani"-ndio kichwa cha maneno cha magazeti ya leo nchini Libanon, huku mabango na biramu yaliyoandikwa kwa lugha za kiarabu, kifaransa, kijerumani na kingereza yametundikwa majiani yakiwa na maandishi yasemayo kwa mfano "Ni ushahidi dhahiri wa jinsi anavyolipenda eneo la Mashrik".

Mizinga 21 itafyetuliwa kwa hishma yake mara tu Papa Benedikt wa 16 atakapowasili uwanja wa ndege na kupokelewa na viongozi wa Libanon, akiwemo pia rais Michel Suleiman-kiongozi pekee wa ulimwengu wa kiarabu ambae ni mkristo.

Katika ziara yake hii ya pili katika eneo la mashariki ya kati, baada ya ile ya mwaka 2009 katika "ardhi takatifu", Papa Benedikt  wa 16 anatarajiwa kuhutubia  angalao mara sabaa. Atawakabidhi maaskofu wa eneo hilo "Nasaha" iliyoandaliwa mwaka 2010 na kusimmiwa na yeye mwenyewe Papa Benedikt wa 16-inayotoa muongozo wa kile kinachostahiki kufuatwa na kanisa katoliki katika eneo la Mashariki ya Kati.

Papa Benedikt wa 16 na mtumishi wake Paolo GabrielePicha: Reuters

Tukio la kusisimua linatarajiwa kuwa mkutano wa Papa Benedikt wa 16 na vijana wa kiislamu na kikristo kesho huko Bkerke,makao makuu ya uongozi wa kanisa la Maronite.

Kwa mujibu wa waandalizi, wajumbe wa kikristo wa Palastina, Misri, Cyprus, Jordan, Iraq na Syria wanatazamiwa kuhudhuria hafla hiyo.

Ziara ya Papa Benedikt wa 16 itamalizika jumapili ijayo kwa misa ya hadhara katika uwanja mashuhuri wa Waterfront mjini Beirut.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Miraji Othman