1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walibya waadhimisha mwaka mmoja wa vuguvugu la kumng´oa Gaddafi

20 Februari 2012

Libya yaadhimisha mwaka mmoja tangu kuanza kwa maandamano ya liyomuangusha Rais Muamer Gadhafi, kwa kufyatua baruti na kutembeza mabango mitaani, wakati kiongozi wao mpya akiapa kulinda amani na utulivu.

Libya yaadhimisha mwaka mmoja wa vuguvugu la kumng´oa Gaddafi.
Libya yaadhimisha mwaka mmoja wa vuguvugu la kumng´oa Gaddafi.Picha: picture alliance/dpa

Waasi waliosaidiwa na Muungano wa Majeshi ya NATO kumuondoa Kanali Muamer Gadhafi kinguvu mamlakani wameweka vizuizi katika mji mkuu Tripoli, Benghazi, mji wa Mashariki ambao ndio kitovu cha vuguvugu hilo, mji wa Magharibi Misrata na miji mingine midogo.

Watawala wapya wa Libya hawajaandaa sherehe zozote rasmi katika ngazi ya kitaifa kama ishara ya kuwatambua na kuwaheshimu maelfu ya watu waliouwawa katika machafuko hayo, yaliyosababisha kukamatwa na kuuwawa kwa Gadhafi tarehe 20 mwezi Oktoba.

Akielezea shamrashamra zinazoendelea mjini Benghazi, Mkuu wa usalama katika viwanja vya Tahrir, Omar Farraj, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa kuwa wameyaita majeshi maalum kutoka nje ya Benghazi na kuyapa jukumu la kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika maadhimisho hayo.

Ghasia hizo ziliharibu mali na majengo nchini Libya.Picha: picture alliance/dpa

Wanawake, wanaume na watoto wamesafiri kutoka mitaa mbalimbali ya nchi na kuwasili jana usiku katika viwanja vya Tahrir, tayari kwa maadhimisho ya kuuangusha utawala wa miaka 42 wa kiongozi huyo wa kiimla.

Baadae leo, wakazi wa Benghazi wakiongozwa na mtawala mpya Mustafa Abdel Jalil na Waziri Mkuu wa muda, Abdel Rahim al- Kib, watakuwa na hafla pamoja na vigogo wengine.

Abdel Jalil amesema Walibya wote wanakaribishwa katika sherehe hiyo na ameonya kumshughulikia yeyote atakayejaribu kuvunja amani. Amesema Thuwar, jeshi la wanamapinduzi linashikilia doria na liko tayari kukabiliana na shambulizi la aina yoyote.

Mkazi mmoja wa Tripoli, Naima Misrati amesema askari wa usalama barabarani na waliokuwa waasi wamekuwa wakisambaza vipeperushi vinavyowaonya watu kufanya mashambulizi vikisema " Hatuwezi kumrejesha Gadhafi kutoka kaburini, lakini tunaweza kukupeleka alipo".

Mmoja wa waasi akipiga teke kikaragosi cha Gaddafi.Picha: dapd

Hatahivyo, Libya bado inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo kuwadhibiti wanamgambo waliopambana na Gadhafi sanjari na kuunda utawala wa sheria.

Uzalishaji wa mafuta, ambacho ni kitega uchumi kikuu cha Libya, umekwama, makazi, biashara, viwanda, shule na hospitali zimeteketezwa katika ghasia hizo zilizosababisha pia maelfu ya raia kufariki dunia

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiwemo Amnesty International, Human Rights Watch na Madaktari wasiokuwa na Mipaka (MSF)yamewashutumu wanamgambo wa Libya kwa kuwatesa wafungwa wao, wengi wao wakiwa ni wapiganaji waliokuwa wakimtii Gadhafi.

Mwandishi: Pendo Paul\AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman