Walibya wapiga kura
7 Julai 2012
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema leo asubuhi na vitafungwa baada ya saa 12 jioni. Uchaguzi huo huenda ukawa tofauti kabisa kwa wakaazi wa mji wa Tripoli, mji ambao umekuwa tulivu kuliko miji ya upande wa mashariki ya Libya ambayo imekumbwa na kuzuka mara kwa mara kwa ghasia mbaya na vitisho vya kuvuruga uchaguzi huo.
Siku ya Ijumaa , helikopta moja ilishambuliwa kwa bunduki mashariki ya Libya na kumuua mfanyakazi mmoja wa tume ya uchaguzi. Ian Martin, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya , amewataka wapigaji kura wote kutumia fursa hii ya kidemokrasia waliyoipata kwa kazi ngumu kuwachagua wawakilishi wa baraza la congress, wakati akishutumu pia mashambulizi lililoomwaga damu.
Kundi linaloshughulikia mizozo lenye makao yake makuu mjini Brussels limeonya kuwa hatua za uchaguzi nchini Libya zinahatarishwa na wapinzani wenye silaha ambao wanatishia kuvuruga uchaguzi huo katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.
Shughuli za uchimbaji mafuta zasitishwa
Pia wakati wa kuelekea kufanyika uchaguzi huo , maeneo matano ya uchimbaji mafuta yamelazimishwa kusitisha uzalishaji na makundi ya watu wenye silaha ambao wanataka uwakilishi mkubwa zaidi kwa maeneo ya mashariki katika bunge litakalochaguliwa lenye wajumbe 200.
Waandamanaji wenye silaha Jumapili iliyopita walivamia ofisi ya tume ya uchaguzi na kuharibu vitu mjini Benghazi. Katika mji wa jirani wa Ajdabiya watu walichoma moto bohari lililokuwa limehifadhiwa vifaa vya kupigia kura.
Muundo wa bunge
Muundo wa bunge umekuwa ni suala linalozusha mjadala mkubwa, wakati makundi ya kisiasa kama lile linalopendelea mfumo wa shirikisho likitaka viti zaidi.
Baraza la taifa la mpito linalotawala NTC, limesema kuwa viti vimegawanywa kwa mujibu wa wingi wa watu katika maeneo, ambapo viti 100 vimepangiwa upande wa magharibi, 60 upande wa mashariki na 40 upande wa kusini.
Lakini makundi upande wa mashariki yanataka mgao sawa wa viti vya bunge na yanatishia kuuchafua uchaguzi wa leo Jumamosi(07.07.2012) iwapo madai yao hayatatekelezwa.
Maafisa wanapuuzia makundi kama hayo kuwa ni ya watu wachache wanaotaka kuchafua, wakieleza kuwa zaidi ya watu milioni 2.7, ama kiasi ya asilimia 80 ya watu wenye haki ya kupiga kura , wamejiandikisha kushiriki katika zoezi hilo la kihistoria.
Walibya hawajawahi kufanya uchaguzi
Libya haijafanya uchaguzi tangu wakati wa enzi za mfalme Idris, ambaye alipinduliwa na Gaddafi katika mapinduzi ambayo hayakumwaga damu mwaka 1969.
Vyama vilipigwa marufuku kuwa ni kitendo cha uhaini wakati wa utawala wa miaka 42 ya kidikteta ya kanali Gaddafi. Kwa hivi sasa kuna vyama 142 ambavyo vimeweka wagombea wao.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Stumai George