1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimu Kenya waamriwa kuripoti shuleni ifikapo Septemba 28

Shisia Wasilwa23 Septemba 2020

Tume ya Kuwaajiri Walimu nchini Kenya, TSC imewaagiza walimu wa shule za msingi na sekondari kurejea shuleni ifikapo Septemba 28 kabla ya tarehe ya kufunguliwa kwa shule kote nchini humo kutangazwa.

Afrika Coronavirus Pandemie / Kenia
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Nancy Macharia amesema walimu wamejiandaa kufidia muda uliopotezwa kati ya mwezi Machi hadi sasa. Wakati huo huo, wizara ya elimu imevitaka vyuo vikuu kuharakisha ukarabati kama sehemu ya kujiandaa kuvifungua.

Macharia alisema hayo, wakati alipokutana na wadau wa elimu kwenye kongamano lililoandaliwa na Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha. Magoha, ambaye amekuwa akilikwepa suala la kufunguliwa shule amesema kuwa huu ni wakati mwafaka wa kuwarejesha watoto shuleni.

Hata hivyo, waziri huyo hakutaja siku ambayo shule zitafunguliwa huku akielezea kuwa mipango iko mbioni ya kufanya hivyo. Kikao cha mawaziri wa elimu, Usalama wa Taifa, Fred Matiang'i na Afya, Mutahi Kagwe, kitafanyika siku ya Ijumaa na kutangaza tarehe ambayo shule zitakapofunguliwa. Lakini suala la kudumisha usalama wa wanafunzi lingali ni changamoto.

Soma pia: Majaribio ya chanjo ya COVID-19 yaidhinishwa Kenya

"Kwa hivyo tunawaomba walimu wetu waripoti shuleni Jumatatu tarehe 28 Septemba, ili kujiandaa kabla ya shule kufunguliwa.” Amesema Macharia

Waziri wa Elimu Kenya Profesa George Magoha (kushoto) asema wameafikiana kuhusu ratiba ya shule. Ilobakia sasa ni Rais Uhuru Kenyatta kutangaza tarehe ya shule kufunguliwa.Picha: imago images/photothek

Serikali imeahidi kuwapa wanafunzi wasio na uwezo wa kiuchumi barakoa, pindi shule zitakapofunguliwa. Aidha, shilingi bilioni 1.9 za Kenya zimetengwa ili kutengeneza madawati ambayo yatasaidia kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona. Hata hivyo, agizo la Tume ya Kuwaajiri Walimu, halijapokelewa vyema na baadhi ya walimu ambao wanasema hawako tayari, kwani hawajapokea mishahara yao.

Shule kuunda kamati za COVID-19

Shule zitahitajika kuunda kamati za COVID-19, juma la kwanza shule zitakapofunguliwa. Taasisi za elimu ambazo zilikuwa zikitumika kama vituo vya kuwatenga wagonjwa wa COVID-19, zimetakiwa kufungwa na kunyunyiziwa dawa kabla wanafunzi hawajarejea shuleni. Wadau kwenye sekta ya elimu, wamekuwa wakifanya vikao kabla ya tarehe ya shule kufunguliwa, kutangazwa. 

COVID-19 yapandisha bei ya ndimu na malimau Kenya

02:27

This browser does not support the video element.

"Nataka kuwafahamisha kuwa leo asubuhi, tumeafikiana, kuhusu ratiba ya shule. Mapendekezo hayo tutayafikisha kwenye kamati kuu, halafu rais atatangaza siku ambayo shule zitafunguliwa.” Amesema Profesa Magoha.

Wakati huo huo, wizara ya elimu imevitaka vyuo vikuu, kuharakisha maandalizi ya kuvifungua vyuo hivyo. Katibu Mkuu katika wizara hiyo, Simon Nabukwesi, amesema kuwa vyuo vitafunguliwa kwa kuzingatia vile ambavyo vimetimiza masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya. Ni vyuo vichache vikuu, ambavyo vimetimiza masharti hayo, huku masomo yakiendeshwa kwa njia ya mtandao.

Mwishoni mwa mwezi huu, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutoa mwongozo mpya wa kufungua uchumi ambao umekuwa ukidororora. Aidha, hotuba yake itagusia mustakabali wa sekta ya elimu. Visa vya maambukizi ya virusi vya corona vimekuwa vikipungua siku baada ya siku, hali ambayo huenda imechangia serikali ya Kenya kupanga kuzifungua teba taasisi zake za elimu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW