1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimu na Madaktari wa Zimbabwe wagoma

21 Juni 2022

Watumishi wa sekta ya afya na elimu nchini Zimbabwe wameanza mgomo wa nchi nzima siku ya Jumatatu.

Simbabwe Corona-Pandemie | Lockdown geplant
Picha: Wanda/Xinhua/imago images

Wanaoshiriki mgomo huo ni madaktari, wauguzi na walimu wanaolalamikia kuanguka kwa thamani ya mishahara yao kutokana na mzozo mkubwa wa kifedha unaoiandama Zimbabwe.

Wauguzi wa nchi hiyo wanalipwa dola 18,000 za Zimbabwe kwa mwezi lakini hivi sasa kiwango hicho ni sawa na dola 55 pekee za Marekani.

Mishahara ya walimu ndiyo yenye nafuu kidogo na inafikia dola za Marekani 75 pekee .

"Ukweli ni kwamba wafanyakazi wanalipwa ujira mdogo. Wafanyakazi wanahangaika kutimiza mahitaji yao" amesema Tapiwanashe Kusotera, kiongozi wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Zimbabwe.

Hapo Jumatatu wafanyakazi wa sekta hiyo waliandamana mbele ya ofisi za Bodi ya Huduma za Afya zilizopo kwenye moja ya hospitali kubwa kabisa nchini humo, wakiwa wamebeba mabango na kuimba nyimbo za malalamiko.

Ahadi ya nyongeza ya mshahara bado kizungumkuti 

Polisi wa kutuliza ghasia walitumwa kwenye eneo hilo huku wagonjwa wakigaragara kwenye viambaza vya majengo hayo bila msaada wowote.

"Bodi yetu ya huduma za afya, ambayo ndiyo mwajiri wetu, na Wizara ya Afya wamekataa katakta kuzungumza na wafanyakazi wa afya" amekaririwa akisema mkuu wa Jumuiya ya Wauguzi nchini Zimbabwe, Enock Dongo.

Picha: Tafadzwa Ufumeli/Getty Images

Wiki iliyopita serikali ya Zimbabwe ilisema itaongeza maradufu mishahara ya watumishi wote wa umma, lakini Dongo amesema hakuna barua yoyote waliyopokea kuhusu dau hilo.

"Hauhitaji kuambiwa kuwa mshahara unaopokea hautoshi" amesema Dongo. "Kwa sasa iko wazi kwamba wajumbe wote wanataka kuacha kazi zao".

Kwa upande wao walimu waliitisha mgomo wa siku tano, kulingana na taarifa iliyotolewa na Chama cha Walimu wa vijijini nchini Zimbabwe.

"Hatuwezi kuendelea kuwa fedheha mbele ya jamii yetu kwa sababu ya umasikini ambao serikali inaamini unapaswa kuwa sehemu ya maisha yetu ya kazi",  taarifa hiyo imesema.

Hata kabla ya mgomo huo wagonjwa kwenye hospitali za umma nchini Zimbabwe tayari walikuwa wakilazimika kununua mahitaji yao wenye ya matibabu na kupeleka kwenye wadi ambazo zimetelekezwa na serikali kwa muda mrefu.

"Hospitali ilitutaka tununue hado glavu, bandeji na dawa za maumivu kwa ajili ya dada yangu lakini hivi sasa wauguzi pia wameondoka" amesema ndugu wa mgonjwa mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Mfumuko wa bei na mzozo wa kifedha chanzo cha kuanguka thamani sarafu ya Zimbabwe 

Picha: AP

Chanzo cha matatizo yote ya kifedha nchini Zimbabwe ni matokeo ya mfumuko mkubwa wa bei ulioangusha thamani ya sarafu.

Mfumuko wa bei ulifikia asilimia 131 mwezi Mei na kufufua kumbukumbu za mfumuko mbaya kabisa wa bei ulioikumba nchi hiyo muongo mmoja uliopita.

Bei za bidhaa zilipanda kiasi kwamba Benki Kuu ya nchi hiyo ililazimika kuchapisha noti ya dola trilioni 100 kuwapunguzia mzigo wanunuzi.

Wakati huo serikali iliamua kuachana na sarafu ya nchi hiyo na kuanza kutumia dola ya Marekani na randi ya Afrika Kusini kama sarafu za malipo.

Lakini mnamo mwaka 2019 serikali ilitangaza kurejesha tena matumizi ya dola ya Zimbabwe lakini tangu wakati huo imekuwa ikiporomoka thamani siku hadi siku.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW