1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine: Walimu wasaidia watoto katika maeneo yaliyokaliwa

9 Januari 2024

Baada ya Urusi kuivamia na kuyahodhi baadhi ya maeneo ya Ukraine kinyume cha sheria, walimu wengi walilazimishwa kufanya kazi nchini Urusi na kufuata mitaala yao. Baadhi wanatumia mbinu za siri kukiuka maagizo haya.

Ukraine Kharkiv | Wanafunzi | Darasa la reli ya chini ya ardhi
Walimu wakianza masomo katika siku ya kwanza ya shule kwenye mkoa wa Kharkiv. Darasa hili limejengwa kwenye reli inayopita chini ya ardhi ili kujilinda na mashambulizi ya UrusiPicha: Madeleine Kelly/ZUMAPRESS.com/dpa/picture alliance

Wazazi na walimu katika maeneo yaliyonyakuliwa na Urusi nchini Ukraine hukabiliwa na vitisho wanapokataa kufuata sera mpya ya elimu iliyoanzishwa na Moscow. Sera hiyo inawalazimisha walimu kufanya kazi nchini Urusi na kulingana na mtaala wa nchini humo, ambao pia unajumuisha vitabu vipya vya historia vinavyohalalisha vita vya Ukraine. Ikumbukwe Urusi iliivamia Ukraine Februari, 2022 na mwezi Septemba, ilitangaza kuyanyakua maeneo manne ya Ukraine ya Zaporizhzhia, Kherson, Donetsk and Luhansk.

Soma pia: Umetimia mwaka mmoja tangu Urusi ilipoamua kuyanyakua maeneo manne ya mashariki ya Ukraine

Mwalimu mmoja wa Ukraine, ambaye pia ni mama wa mwanafunzi mdogo asubuhi ameiambia DW kwamba mwanane huwa anakwenda shule, ambako huwa hu lazimishwa kuzungumza kirusi kwa wanafunzi na kuwafundisha kwa vitabu vya lugha ya kirusi. Lakini amesema jioni, huwa wanawafundisha kwa Kiukraine kwa njia ya mtandao na kuwafunza mambo ya kwao.

Masuala ya lugha ya Kirusi na Kiukrein, historia na utambulisho yamekuwa kitovu cha mzozo hata kabla ya uvamizi huu. Mamilioni ya raia wa Ukraine wanazungumza Kirusi kama lugha yao ya kwanza. Baada ya vuguvugu la Euromaidan: Wimbi la maandamano na ghasia nchini Ukraine, lililoanza Novemba 21, 2013 katika Uwanja wa Uhuru (Maidan) huko Kyiv, taifa hilo  ilipitisha sheria zinazoamuru matumizi makubwa ya Kiukreni ikiwa ni pamoja na shuleni, kwenye televisheni, na miongoni mwa wafanyakazi wa sekta ya umma.

Elimu kama 'kifaa cha kusambaza propaganda'

Ripoti ya Disemba 2023, ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International linaituhumu Urusi kwa kugeuza "elimu na kuwa chombo cha kusambaza propaganda na kujaribu kutokomeza utamaduni, urithi na utambulisho wa Kiukreni.

Soma pia: Jeshi la Ukraine lavuka na kuingia katika jimbo la Kherson

Rais Vladimir Putin aliwaagiza wanajeshi wake kuivamia Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari, 2022Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Kwa sasa Moscow inadhibiti chini ya asilimia 18 ya eneo la Ukraine, ikiwa ni pamoja na Rasi ya Crimea iliyotwaliwa mwaka 2014, hii ikiwa na kulingana na makadirio ya Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita. Amnesty International imeinukuu Wizara ya Elimu ya Ukraine ikisema hadi Disemba 2022, takriban vituo 918 vya elimu kwa watoto wenye umri wa miaka 6-17 vilikuwa katika maeneo yaliyokaliwa.

Walimu wanatumia mbinu za msituni

Baadhi ya walimu wanaouhofia utawala wa Urusi, baadhi ya wanafunzi na wazazi walianza "kuchimba mashimo kwenye bustani zao ili kuficha kompyuta zao na simu za mkononi ama kujificha kwenye vyumba vya kulala na pengine kwenye vibanda vilivyotumika zamani ili kupata mawasiliano na kusoma kwa njia ya mtandaoni kwa lugha ya Ukreini, limesema Amnesty.

Soma pia: Ukraine: Putin azuru mikoa miwili inayokaliwa na Urusi

Shirika hilo lilizungumza pia na mkutubi mmoja aliyesema alilazimika kukutana kwa siri na wanafunzi na kuwapa vitabu kwa kuwa wanajeshi wa Urusi huwa katika doria kila wakati na kufanya upekuzi wa kiholela kwenye vijiji vyao. Hii ni sehemu tu ya mtindo mpana wa vitisho kutoka kwa wanajeshi hao. Maafisa wa Urusi pia hutumia vitisho kwa kuchukua watoto kutoka kwa wazazi ili kuhakikisha kufuata sheria.

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limesema ni vigumu kwa raia wa Ukraine kusoma kwa luigha yao katika maeneo yanayokaliwaPicha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Amnesty imesema, mama mmoja aliyekataa kumpeleka shule mtoto wake wa miaka 15 alisema kuna siku wanaume waliokuwa wamevalia sare za Urusi, walimvamia na kumwambia ikiwa hatampeleka mtoto wake shuleni, basi watampeleka kwenye kituo cha watoto yatima nchini Urusi. Mtoto huyo alikuta shule ikiwa imepambwa na alama zinazoashiria Urusi huku wanajeshi wenye silaha wakiwa wamepiga kambi nje ya mlango na ndani ya jengo.

Urusi kuchunguza wanaotumia VPN.

Alipozungumza na DW, mwanaharakati Violeta Artemchuk alisema kwamba tovuti zote zilizokuwa zinatoa huduma ya masomo kwa njia ya mtandaoni nchini Ukraine wamezuiwa na wanaweza kufanya hivyo kwa kutumia VPN.

Amesema wavamizi wanachunguza sana vifaa vyote vinavyotumiwa na watoto na wazazi ili kujua ni nani bado anaendelea kusoma kwenye shule za Ukraine.

Valentina Potapova mzaliwa wa Crimea, ambaye ni mkuu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Almenda ametoa wito kwa Ukraine kuandaa shule ya mtandaoni maalumu kwa ajili ya watoto waliopo kwenye maeneo yanayokaliwa. Shule kama hiyo ingewaruhusu watoto kusoma Kiukreni, historia na sheria.

Akiongea na DW, Potapova amesema pendekezo hili limekuwa likipigwa danadana tangu Urusi ilipoinyakua Crimea mwaka 2014 na kuundwa kwa serikali haramu zinazoiunga mkono Urusi huko Donetsk na Luhansk. Hata hivyo, kwa vile Kyiv haijatekeleza hatua hii, Ukraine imepoteza kizazi kizima cha watoto katika muongo mmoja uliopita.

Soma pia: Putin kubaki madarakani milele?