1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinda amani wapelekwa Afrika ya Kati kulinda uchaguzi

19 Desemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande zote kukomesha haraka vitendo vya uhasama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi wa rais Desemba 27

Zentralafrikanische Republik UN Soldaten
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataufa amelaani ongezeko la machafuko na kuzitaka pande zote kufanya kazi ya kuhakikisha kuna mazingira bora ya kuandaa uchaguzi halali, unaozijumuisha pande zote na wenye amani mnamo Desemba 27.

Makundi matatu makuu ya wapiganaji -- ambayo yanadhibiti thuluthi mbili ya Jamhuri ya Afrika ya Kati -- yamemtishia Rais Faustin Archange Touadera, yakimtuhumu kwa kupanda wizi wa kura ili kushinda muhula wa pili.

Rais Touadera anatafuta muhula wa pili madarakaniPicha: Camille Laffont/APF/Getty Images

Mivutano imeongezeka nchini humo, huku serikali ikiimshutumu rais wa zamani Francois Bozize kwa kuwa na mpango wa kuidhoofisha nchi, wakati nao upinzani nao ukisema unahofia kutokea udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa rais na bunge.

Touadera, 63, anapigiwa upatu katika kinyang'anyiro cha rais chenye wagombea 17. Bozize alirejea nchini Desemba 2019 akitokea uhamishoni alikoishi kwa miaka mingi na anatuhumiwa na serikali kwa kuiyumbisha nchi.     

Bozize, 74, bado ana ufwasi mkubwa katika upande wa kaskazini magharibi, hasa miongoni mwa kabila la Gbaya, ambalo ndilo kubwa Zaidi nchini humo, na lina wafuasi wengi jeshini.

Bozize wakati akiwa rais mwaka wa 2011Picha: JOHN THYS/AFP/Getty Images

Jaribio la Bozize kugombea lilizuiwa na mahakama ya juu nchini humo mnamo Desemba 3 kwa sababu anatafutwa katika waranti wa kimataifa wa kumkamata uliowasilishwa 2014 na Jamhuri ya Afrika ya Kati kuhusu mashitaka yakiwemo mauaji, ukamataji wa kiholela na mateso. Bozize anasema anakubali uamuzi wa mahakama na ametangaza kumuunga mkono waziri mkuu wa zamani Anicet-Georges Dologuele.

Nchi hiyo ilitumbukia katika mgogoro 2013, wakati rais wa wakati huo Francoise Bozize alipoondolewa madarakani na Seleka, muungano wa waasi kutoka jamii ya Waislamu walio wachache.

Mapinduzi hayo yalizusha umwagaji damu kati ya Seleka na kundi la wapiganaji walojiita anti-Balaka, wengi wao wakiwa Wakristo. Ufaransa iliingia kati koloni lake zamani na baada ya kipindi cha mpito, uchaguzi uliandaliwa 2016 na Touadera akashinda.

AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW