1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinzi wa Blackwater wakutwa na hatia

Elizabeth Shoo23 Oktoba 2014

Mahakama moja ya jijini Washington, Marekani imewakuta na hatia walinzi wanne wa kampuni ya Blackwater. Mwaka 2007, walinzi hao waliwaua kwa kuwapiga risasi raia wa kawaida wasiopungua 14 nchini Iraq.

Wanajeshi wa Blackwater
Picha: picture-alliance/dpa

Kampuni ya Blackwater ilikuwa imeajiriwa kuwalinda wanadiplomasia wa Kimarekani katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, na katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Tarehe 16 Septemba mwaka 2007 wafanyakazi wanne wa kampuni hiyo walikuwa wakiusindikiza msafara mmoja wa magari mjini Baghdad na waliwafyatulia risasi raia ambao hawakuwa na silaha. Walinzi wa Blackwater walidai kuwa msafara wao ulishambuliwa na ndio maana wakaamua kujibu mashambulizi. Waliuwawa watu wasiopungua 14 na wengine kujeruhiwa. Miongoni mwao walikuwa wanawake na watoto.

Kesi dhidi ya wafanyakazi wa Blackwater iliendeshwa kwa miezi miwili na hatimaye hukumu kutolewa. Wote wanne wamekutwa na hatia katika makosa kadhaa, ikiwepo kosa la kuua kwa kukusudia pamoja na kukiuka sheria za kutumia silaha. Hata hivyo jaji aliyekuwa anaisimamia kesi hiyo bado hajataja tarehe ya kutangaza iwapo watapewa kifungo cha jela au la, na kama watakwenda gerezani, itakuwa kwa muda gani.

Mkataba wabatilishwa

Wakili mmoja wa wahukumiwa hao alisema hukumu hii ni nzito mno akiapa kwamba wataipinga kwa nguvu zote na wanaamini kuwa watashinda. Kwa upande mwingine, mmoja wa majeruhi, Hassan Jabir, alielezea kuridhika na hukumu iliyotolewa. Yeye alilengwa kwa risasi mbili, moja mkononi na nyingine mgongoni. Madaktari walimwambia kuwa itakuwa hatari kuziondoa hivyo zimebakia ndani ya mwili wake.

Maafisa wa Blackwater walikuwa wakiwalinda wanadiplomasia IraqPicha: AP

Mauaji ya mwaka 2007 yalitibua hasira za raia wa Iraq dhidi ya Marekani. Hata hivyo kuna ubishi juu ya kile kilichotokea. Mawakili wa wahukumiwa wanasisitiza kuwa upo ushahidi kwamba wafanyakazi hao wa Blackwater walishambuliwa kwa bunduki na polisi pamoja na wapiganaji, jambo lililowalazimisha wafyatue risasi pia kama namna ya kujihami. Lakini upande wa mashtaka unadai hapakuwa na mashambulizi na kwamba walinzi hao walitumia bunduki zao kiholela ingawa hakuna aliyewachokoza.

Kufuatia kashfa hiyo, Iraq iliifuta leseni ya kampuni ya Blackwater kufanya kazi ndani ya nchi hiyo. Mwaka 2009 ilibadilisha jina lake kuwa Xe Services na miaka miwili baadaye ikajiita Academi. Rais Barack Obama alipoingia madarakani aliubatilisha mkataba wa serikali yake na kampuni ya Blackwater.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap

Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW