1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUturuki

Waliofariki Uturuki pekee kwenye tetemeko wapindukia 40,000

Sylvia Mwehozi
18 Februari 2023

Jumla ya watu waliofariki nchini Uturuki pekee kutokana na tetemeko kubwa la ardhi imepindukia elfu 40,000 kulingana na takwimu ziizotolewa na wizara ya mambo ya ndani. Watu bado wanaokolewa wakiwa hai.

Erdbeben in der Türkei - Kahramanmaras
Picha: Tunahan Turhan/ZUMA/IMAGO

Mamlaka nchini Uturuki zimesema siku ya Ijumaa kwamba, zaidi ya wafanyakazi 35,000 wamejiunga na juhudi za uokoaji kuwasaka manusura wowote takriban siku 12 baada ya tetemeko kubwa la ardhi, huku kukiwa na matumaini kidogo.

Makamu wa Rais wa Uturuki Fuat Oktay aliwaambia waandishi wa habari mjini Ankara kuwa timu za uokoaji zimewatafuta manusura katika majengo takribani 200 yaliyoporomoka katika majimbo 11 ya Uturuki.

Oktay amesema kuwa juhudi za uokoaji zitaendelea "hadi mwisho," na kuongeza kuwa juhudi hizo zimeelekezwa zaidi kwenye mkoa wa Hatay ulioathirika zaidi. Ingawa kumekuwa na ripoti za kufifia kwa matumaini ya kuwapata watu walio hai,  lakini timu za uokozi zimekuwa zikiwaokoa baadhi ya watu walio hai kutoka kwenye vifusi.

Raia wa Syria wakiwa wamesimama kwenye mabaki ya jengo lililoporomokaPicha: Mahmoud Hassano/REUTERS

Katika mji wa Hatay, mwanaume mwenye umri wa miaka 45 ameokolewa akiwa hai ikiwa ni baada ya masaa 278. Mwanaume huyo ameokolewa katika wilaya ya Defne, kulingana na ripoti ya shirika la habari la taifa la Anadolu. Timu za uokoaji zinazofanya kazi usiku kucha, zilifanikiwa kumwokoa mwanamke na wanaume wawili wakiwa hai katika mabaki ya tetemeko la ardhi.

Katika jiji la Antakya, wafanyakazi wa uokoaji wa polisi walimpata mvulana wa miaka 12  anayeitwa Osman akiwa hai baada ya kuopoa miili 17 kutoka kwenye eneo ambalo jengo lililoporomoka.

Maelfu ya watu pia wamepoteza maisha katika nchi jirani ya Syria iliyokumbwa na migogoro, ambapo juhudi za kushughulikia maafa hayo zimetawaliwa na mizozo ya siasa za kimataifa na kutatizwa na miundombinu duni.

Takwimu zilitolewa na shirika la afya duniani WHO Jumapili iliyopita juu ya idadi ya watu waliokufa nchini Syria kutokana na tetemeko ni 5,900.Wengine waokolewa Uturuki baada ya saa 260

Waziri wa mipango ya miji wa Uturuki Murat Kurum alisema siku ya Ijumaa kwamba majengo yapatayo 84,000 yameporomoka au kuharibiwa sana kufuatia matetemeko makubwa mawili ya ardhi. Kurum amesema majengo yaliyoharibiwa yanahitaji kubomolewa haraka, na kuwataka raia kukaa mbali nayo.

Serikali ya Uturuki ilitangaza kwamba itaanza ujenzi mpya wa majengo katika miji kadhaa iliyoathiriwa kuanzia mwezi Machi. Mamlaka za Uturuki zimelaumiwa kwa uzembe wa utekelezaji kanuni za ujenzi, ambazo zinatajwa kuwa huenda zilichangia idadi kubwa ya vifo.

Kulingana na shirika la habari la Anadolu, zaidi ya watu 50 wakiwemo wakandarasi wamekamatwa kuhusiana na majengo yaliyoporomoka.Manusura bado wanaendelea kupatikana kufuatia tetemeko Uturuki na Syria

Misaada ya kimataifa imeendelea kuwasili Uturuki siku ya Ijumaa, huku Tume ya Ulaya ikidai kwamba misaada zaidi, ikiwa ni pamoja na mahema na hita, kwa ajili ya wahanga wa kaskazini mwa Syria itawasilishwa kupitia Uturuki.

Jumla ya malori 178 yaliyobeba msaada kutoka Uturuki kuelekea kaskazini magharibi mwa Syria yamevuka mpaka tangu Februari 9, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa.