1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMalawi

Waliokufa kwa kimbunga Malawi na Msumbiji wapindukia 200

15 Machi 2023

Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Freddy nchini Msumbiji na Malawi imepindukia 200 huku vikosi vya uokozi vikionya uwezekano wa kuwepo wahanga zaidi wa kimbunga hicho wakati vikiendelea kuwatafuta manusura.

Malawi Mosambik Zyklon Tropensturm Freddy
Picha: NASA/AP Photo/picture alliance

Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Freddnchini Msumbiji na Malawi imeripotiwa kupindukia 200, huku vikosi vya uokozi vikionya juu ya uwezekano wa kuwepo wahanga zaidi wa kimbunga hicho wakati vikiendelea kuwatafuta manusura kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na kimbunga hicho. 

Matumaini ya kuwapata manusura yanazidi kupotea kila uchwao. Mamlaka zinasema kazi ya uokozi na kufikisha misaada ya kiutu kwa wahitaji inakabiliwa na vihunzi ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa miundombinu ya barabara kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na maporomoko ya udongo. Kulingana na idara ya kushughulikia maafa ya Malawi karibu watu 19,000 walikuwa hawajulikani walipo hadi jana Jumanne.

"Barabara zinatatiza juhudi za kuwafikia. Kweli watu wanaomba tupeleke helikopta lakini lazima wajue hata helikopta zinahitaji mazingira ya aina fulani ili ziweze kufanya kazi. Lakini tumejaribu kutuma tano. Jeshi liko huko kila wakati. Tuna kituo ambacho tunaweza kuona ni aina gani ya msaada tunaotakiwa kuwapelekea watu." Alisema waziri wa serikali za mitaa nchini Malawi Richard Chimwendo Banda.

Soma Zaidi: Kimbunga Freddy kupiga tena Msumbiji

Mratibu wa mradi wa dharura wa Madaktari wasio na Mipaka, MSF nchini Malawi Guilherme Botelho naye anakiri hali ni ya mashaka katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya majeruhi wapatao 584 ambayo inatarajiwa kuongezeka katika siku zijazo. Amesema watu wengi na nyumba zao wamesombwa na matope katika mji mkuu Blantyre.

Wakazi wa Malawi wakiwa wanavuka kwenye daraja la muda baada ya maeneo mengi kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko.Picha: JACK MCBRAMS/AFP/Getty Images

John Witman, mmoja ya manusura aliyekutwa amesimama eneo kulikokuwa na nyumba ya mkwe wake iliyosombwa na maji anasema anatamani hata wangempata mwanaye na kuongeza kwa huzuni kubwa kwamba wanajiona kama waliotengwa kwa kuwa hawana mtu wa kuwasaidia na matumaini yamepotea kwa kuwa wanachokishuhudia sasa ni miili tu ya watu iliyokwama kwenye tope.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera tayari ametangaza hali ya janga nchini mwake wakati kimbunga hicho kikitarajiwa kuendelea kuyapiga maeneo ya katikati ya Msumbiji na kusini mwa Malawi kikiambatana na mvua kubwa kabla ya kurudi baharini baadae hii leo, hii ikiwa ni kulingana na utabiri kutoka kituo cha masuala ya hali ya hewa cha Umoja wa Mataifa kilichopo katika kisiwa cha Reunion. Manusura wengi sasa wanajihifadhi kwenye majengo ya shule na makanisa.

Nchini Msumbiji taarifa zinathibitisha kwamba watu 20 wamekufa na 24 kujeruhiwa kutokana na kimbunga hicho na nyumba 1,900 kuharibiwa na hasa katika jimbo la Zambezia, lililoko pwani mwa taifa hilo. Maelfu ya watu bado wamekwama kwenye vituo na makazi ya muda kupisha kimbunga hicho kupita.

Kimbunga Freddy kwa mara ya kwanza kiliipiga Madagascar, Februari 21 na kuharibu eneo kubwa la kisiwa hicho kabla ya kufika Msumbiji Februari 24 na kusababisha vifo vya idadi kuwa ya watu kwenye mataifa hayo yote mawili na wengine kama 400,000 wakiwa wameathiriwa kwa namna moja ama nyingine.

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Amnesty International limetoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuhamasisha msaada wa rasilimali na kuunga mkono juhudi za uokozi nchini Msumbiji na Malawi ambayo tayari ilikuwa inapambana na mlipuko wa kipindupindu.

Sikiliza Zaidi: 

14.03.2023 Matangazo Ya Jioni

This browser does not support the audio element.