1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa kwa mafuriko, maporomoko Kenya wapindukia 160

30 Aprili 2024

Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia mafuriko na maporomoko ya tope yanayosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha nchini Kenya imefikia 169, huku wengine 200,000 wakiachwa bila makaazi.

Kenya Nairobi | Mafuriko
Mafuriko yaendelea kuikumba Kenya.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Kwenye taarifa yake, Wizara ya Usalama wa Taifa ilisema siku ya Jumanne (Aprili 30) kwamba Kaunti za Nairobi, Tana River, West Pokot, Nakuru na Muranga ndizo zilizoathiriwa zaidi na mafuriko hayo.

Kufuatia hali hiyo, Rais William Ruto alitazamiwa kufanya kikao cha dharura na baraza la mawaziri kutathmini mbinu muafaka za kukabiliana na athari yajanga hilo.

Kabla ya kikao hicho, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliyelitembelea eneo la Mai Mahiu alisistiza kuwa wanafanya kila lililo katika uwezo wao kuwasaidia walioathirika.

Soma zaidi: Bwawa lapasua kingo Kenya, watu 45 wapoteza maisha

Takwimu rasmi zilionesha kuwa watu 91 hawajulikani waliko baada ya kupotea kwenye maeneo mbalimbali.

Gavana wa Kaunti ya Nakuru, Susan Kihika, alisema kuwa maporomoko ya tope yaliyotokea eneo la Mai Mahiu yalikuwa yamepoteza maisha ya zaidi ya 40, lakini ilihofiwa kuwa idadi huenda ingeliongezeka wakati juhudi za uokozi na ufuatiliaji zinaendelea.

Kenyatta atoa milioni mbili kusaidia uokozi

Siku ya Jumanne, rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitoa mchango wa shilingi milioni mbili za Kenya kuunga mkono harakati za uokozi za Shirika la Msalaba Mwekundu.

Bwawa lapasua kingo na kusababisha maafa Kenya

02:23

This browser does not support the video element.

Kwenye taarifa yake, kiongozi huyo wa zamani aliwaasa Wakenya kuwa makini katika msimu huu wa mvua ili kuepuka kupoteza maisha na mali.

Soma zaidi: Ruto aitisha kikao maalum kujadili athari za mafuriko

Takwimu za Wizara ya Usalama wa Taifa zilisema kuwa watu wapatao 200,000 walikuwa wameachwa bila makaazi, baada ya nyumba zao kujaa maji.

Mamlaka ya Barabara nchini Kenya (KENHA) iliifunga barabara kuu inayotokea Mai Mahiu kuelekea Narok, baada ya handaki la reli lililojengwa enzi za utawala wa ukoloni kuanza kumimina maji na matope kuelekea kijiji cha Kamuchiri huko Kijabe, jirani na Kaunti ya Kiambu.

Serikali ilitenga sehemu tatu mahsusi kwa wahanga wa mafuriko kupata hifadhi katika kaunti ya Nairobi, kwa ushirikiano na Idara ya Huduma kwa Vijana (NYS).