1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa maandamano ya Sudan wapindukia 20

15 Novemba 2021

Idadi ya waliouawa tangu jeshi kuchukuwa tena madaraka nchini Sudan imefikia watu 23 kufuatia wengine wanane kupoteza maisha ndani ya siku tatu zilizopita, huku raia wakiendelea kuandamana kuupinga utawala wa kijeshi.

Sudan Khartum | Proteste gegen Militärregierung
Picha: AFP/Getty Images

Vijana watatu ni miongoni mwa waliouawa kwenye maandamano ya Jumamosi (Novemba 13), ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkali kabisa kutoka vyombo vya dola tangu jeshi kutwaa madaraka tarehe 25 Oktoba. 

Chama Huru cha Madktari wa Sudan (CCSD) kilisema kuwa idadi ya wahanga waliyoweza kuithibitisha ni 23.

Kikiwataja kwa majina wahanga hao kiliowaita mashahidi, chama hicho kilisema mmoja wao ni "msichana wa miaka 13 ambaye alipigwa risasi ya kichwa akiwa nje ya nyumba yao." 

"Zaidi ya majeruhi 200 wamechunguzwa hadi sasa, wakiwemo 10 waliojeruhiwa kwa risasi za moto. Baadhi ya majeruhi wamepigwa risasi za mpira ama mabomu ya machozi." Ilisema ripoti ya CCSD kwa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa televisheni inayomilikiwa na serikali, maafisa 39 wa polisi walijeruhiwa kufuatia makabiliano hayo ya siku ya Jumamosi.

Kijana akikimbia mashambulizi ya mabomu ya machozi mjini Khartoum.Picha: AFP/Getty Images

Polisi, ambao walikanusha kutumia risasi za moto, waliwatuhumu waandamanaji kwa kushambulia vituo vya polisi, wakidai kuwa maandamano hayo yalianza kwa amani lakini baadaye yakabadili muelekeo.

Maandamano hayo makubwa ya siku ya Jumamosi yalifanyika siku mbili tu baada ya Jenerali Burhani kuangaza serikali yake mpya ya kijeshi, ikichukuwa nafasi ya ile aliyoipinduwa. 

Mkuu wa al Jazeera akamatwa

Katika hatua nyengine, vyombo vya usalama vimeizingira nyumba ya mkuu wa kituo cha utangazaji cha Al Jazeera mjini Khartoum na kumkamata jioni ya jana, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kituo hicho chenye makao yake makuu nchini Qatar. 

Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.Picha: /AP/dpa/picture alliance

Wiki iliyopita, Al Jazeera ilirusha mahojiano ya kwanza na mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah Al Burhani, siku chache kabla ya kujiteuwa mwenyewe kuendelea kushikilia wadhifa wa mkuu wa nchi.

Mnamo tarehe 25 Oktoba, Jenerali Burhani alitangaza hali ya hatari, akaipinduwa serikali ya mpito na kuwatia nguvuni mawaziri wote wa kiraia wa serikali hiyo iliyojumuisha pia wanajeshi. 

Tangu hapo, waandamanaji wamekuwa wakimiminika mitaani licha ya kukatwa kwa huduma za intaneti na kuingiliwa kwa mifumo ya mawasiliano, hali inayowafanya wanaharakati kutegemea ujumbe mfupi wa maneno kwa simu na michoro ya grafiti kusambaza taarifa za maandamano.

Serikali mpya aliyoitangaza Jenerali Burhani katikati ya wiki inajumuisha mawaziri kutoka jeshini na wajumbe wa makundi ya zamani ya waasi katika serikali iliyopinduliwa, na pia raia kadhaa wasiofahamika sana, ambao wanachukuwa nafasi ya wajumbe wa muungano wa makundi ya kiraia, Forces for Freedom and Change, ulioongoza maandamano ya umma ya mwaka 2019 yaliyomng'owa Rais Omar Hassan Al Bashir.