1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walioteswa Belarus wamshtaki Lukashenko Ujerumani

12 Mei 2021

Watu 10 wamewasilisha malalamiko ya jinai dhidi ya kiongozi wa Belarus, Alexander Lukashenko kwa madai ya utesaji na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. DW imezungumza na waathirika wawili kati ya 10 walioteswa nchini humo. 

Weißrussland Minsk | Festnahmen während Demonstration
Picha: AP/picture alliance

Valery Samolasow anakumbwa na kiwewe kila siku. Ameiambia DW kwamba hawezi kupata usingizi na ameandikiwa dawa za kumsaidia kutopata msongo wa mawazo na kuweza kulala. Samolasow anasema vidole vyake vina ganzi tangu alipoteswa. 

Amesema amekuwa na wakati mgumu kuzungumzia jinsi alivyopigwa na kudhalilishwa. Mwaka 2020 Samolasow alikuwa akifanya kazi kama mtaalamu wa Mawasiliano ya Teknolojia nchini Uingereza. Majira ya joto mwaka huo alikwenda Belarus kutafuta nyaraka za kumruhusu kufanya kazi na kupiga kura katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Baada ya maafisa wa uchaguzi kumtangaza Alexander Lukashenko mshindi, siku iliyofuata yalizuka maandamano ya nchi nzima kupinga ushindi wake, hatua iliyosababisha kukamatwa kwa baadhi ya waandamanaji akiwemo Samolasow. Alikamatwa akiwa njiani kwenda kumtembelea rafiki yake katikati ya mji wa Minsk Agosti 10.

Valery Samolasow baada ya kuachiwa huruPicha: Valery Samalazau/privat

Anasema ukatili dhidi yake ulikuwa mkali katika kituo cha polisi na kwenye gari la kusafirisha wafungwa. Watu wengi walipiga kelele, walilia, walisali na wengine walitapika. Anasema alipoteza fahamu mara mbili kutokana na maumivu. Samolasow alishikiliwa kwa muda wa saa 84 kabla ya kuachiwa huru.

Kwa upande wake Kacper Sienicki, mwandishi habari wa kujitegemea wa Poland, alikamatwa katikati ya Minsk Agosti 10. Ameaimbia DW alikuwa akitembea pamoja na mpiga picha ambaye ni rafiki yake. Anasema bila kutarajia walipelekwa kwa kutumia basi hadi kwenye gari la polisi na kisha kuhamishiwa kwenye kituo cha polisi. 

Mateso waliyopitia waathirika

Walipofika walipigwa na kutukanwa kutokana na utaifa wao. Walishtakiwa kwa kuwa vibaraka, kuchochea harakati za maandamano na kuandaa mapinduzi. Sienicki ambaye alikuwa anaishi Warsaw, alikwenda Belarus kuripoti kuhusu uchaguzi wa rais kwa ajili ya wafuatiliaji wa Poland. Alishikiliwa kwa muda wa saa 72 kabla ya kuachiwa huru.

Samolasow na Sienicki ni miongoni mwa watu kumi ambao wamewapa mawakili wa Ujerumani jukumu la kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Rais Lukashenko. Wanamshutumu kwa kuviamuru vikosi vya usalama kutumia nguvu kufanya ukandamizaji dhidi ya raia na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Mawakili hao wanasema watu 10 waliteswa wakati walipokamatwa.

Mwandishi habari wa Poland, Kacper SienickiPicha: Privat

Kutokana na hatua za kisheria kutochukuliwa ndani ya Belarus kwenyewe dhidi ya maafisa wa usalama au Lukashenko, mawakili wana matumaini kesi huru inaweza kufunguliwa katika mahakama ya Ujerumani. Wananchi wa Belarus wanaoishi Ujerumani wamerekodi zaidi ya visa 100 vya ghasia na manyanyaso dhidi ya waandamanaji wa upinzani.

Watu hao 10 wanataka kuiona serikali ya Lukashenko ikiwekwa kwenye kundi la utawala wa kigaidi. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, takriban madai 1,800 yamefunguliwa na waathirika nchini Belarus kutokana na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji. Hakuna kesi hata moja iliyofunguliwa mahakamani. 

Wakati huo huo, nchi za Ulaya zilianza kushughulikia kesi hizo za uhalifu. Mbali na Ujerumani, madai mengine pia yamefunguliwa Lithuania, Poland na Jamhuri ya Czech na nchi hizo zinapanga kuchukua hatua za kisheria kutokana na mwenendo wa serikali ya Belarus.

(DW https://bit.ly/3ohqrSz)