1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliotoroka karantini Zimbabwe na Malawi wasakwa

28 Mei 2020

Msako umeanzishwa baada ya mamia ya watu kutoroka vituo vya karantini katika nchi za Zimbabwe na Malawi huku maafisa wakihofia kuwa watasambaza maambukizi hayo katika mataifa ambayo mifumo yake ya afya huenda ikalemewa.

Südafrika Corona-Pandemie Soldaten
Picha: picture-alliance/dpa/J. Delay

Nchini Malawi, zaidi ya watu 400 ambao walirejeshwa nchini humo hivi majuzi kutoka Afrika Kusini na kwengineko, walitoroka kituo kimoja katika uwanja wa michezo mjini Blantyre kwa kuruka ua ama kutoka katika milango mikuu ya uwanja huo uliopo chini ya uangalizi wa maafisa wa polisi na wahudumu wa afya.

Polisi na wahudumu hao wa afya wamewaambia wanahabari kuwa hawakuweza kuwazuia kwasababu ya ukosefu wa vifaa vya kinga.Baadhi ya waliotoroka waliwaambia wanahabari kuwa waliwahonga maafisa wa polisi. Watu 46 kati yao walithibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi hivyo.

Nchini Zimbabwe, msemaji wa polisi Paul Nyathi, amesema kuwa maafisa wa polisi wanawasaka zaidi ya watu 100 waliotoroka kutoka vituo hivyo ambapo kuna agizo la lazima la kuwa chini ya karantini kwa siku 21 kwa wale wanaoingia nchini humo kutoka ng'ambo.Nyathi anasema kuwa watu hao walitoroka na kuingia vijijini na kwamba wanawaonya watu kutowapa hifadhi na kuongeza kuwa watu hao waliotoroka wanaendelea kuwa tishio kubwa kwa jamii.

Wakazi wa Afrika Kusini walioathirika na janga la COVID-19 wapokea chakula cha msaada Picha: picture-alliance/AP/T. Hadebe

Takriban visa vyote 75 vipya vya maambukizi nchini Zimbabwe wiki hii ni vya kutoka katika vituo vinavyowashikilia mamia ya watu waliorejea nchini humo, wakati mwingine sio kwa hiari kutoka mataifa jirani ya Afrika Kusini na Botswana.Waziri wa afya Obadiah Moyo, ameiambia kamati maalumu ya bunge wiki hii kwamba vituo hivyo vya karantini vimekuwa vyanzo vya hatari.

Aliyekuwa waziri wa habari wa Zimbabwe Monica Mutsvangwa, siku ya Jumatano aliwaambia wanahabari kwamba serikali inaimarisha usalama katika shule, vyuo na mahoteli zinazotumika kama vituo vya karantini. Msemaji wa serikali Nick Mangwana, alipendekeza kuwa maafisa wa usalama wanaolinda vituo vyenye kuta ndefu huenda wanapokea hongo kuwaruhusu watu kuondoka mapema.

Serikali ya Zimbabwe yatoa onyo

Serikali ya Zimbabwe pia ina wasiwasi kuhusu watu wanaovuka mipaka yenye mianya na kukosa kufika katika vituo vya karantini.Wizara ya habari, imeanza kutoa nambari za dharura na kuwataka watu kukoma kuwahifadhi waliovuka mipaka kinyume cha sheria na wale wanaotoroka karantini.

Malawi pia ilishuhudia kisa kingine cha kutoroka kwa watu mapema wiki hii wakati watu 26 walipoondoka katika kituo cha mpakani cha Mwanza walipokuwa wakisubiri majibu ya uchunguzi wao. Watu wanaowasili nchini humo wanakabiliwa na siku 14 za kuwa chini ya karantini.

Mkurugenzi wa wilaya wa afya na huduma za kijamii mjini  Blantyre Gift Kawalazira, amesema kuwa walilemewa wakati zaidi ya watu elfu 2 walipofika katika kituo hicho cha mpakani mjini Mwanza mwishoni mwa juma na kwamba kuwazuia baadhi katika uwanja huo ulikuwa uamuzi wa mwisho baada ya mipango ya kutumia taasisi za elimu kushindwa kutokana na ukosefu wa fedha.

Kawalazira ameongeza kusema kuwa watu wanapaswa kuelewa kuwa kuwekwa chini ya karantini sio adhabu lakini ni kwa ajili ya kulinda umma kwa ujumla. Hatua kidogo za kuzuia watu zilionekana katika uwanja huo huku watu wakitoka na kutembea huru kununua chakula kutoka kwa wauzaji walioko karibu. Watu hao waliwaambia wanahabari kuwa hawajapokea chakula chochote kutoka kwa mamlaka tangu siku ya Jumatatu.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW