1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouawa kwa mashambulizi ya Israel wafikia 3,785 Gaza

20 Oktoba 2023

Israel imeendeleza mashambulizi dhidi ya kundi la Hamas usiku kucha katika Ukanda wa Gaza na hadi sasa idadi ya vifo imefikia watu 3,785.

Gazastreifen | Zerstörung nach Luftangriffen im Jabalia Camp, Gaza
Hali ilivyo kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia, Ukanda wa Gaza, katika picha iliyochukuliwa tarehe 11 Oktoba 2023.Picha: YAHYA HASSOUNA/AFP/Getty Images

Jeshi la Israel limesema ndege zake za kivita zilishambulia maeneo zaidi ya 100 na kumuua mwanachama mmoja wa Hamas ambaye inaaminika huenda alishiriki katika uvamizi wa Oktoba 7 uliosababisha vifo vya watu 1,400 nchini Israel.

Kwa upande mwengine, mamia ya watu waliindamana siku ya Alkhamis (Oktoba 19) mjini New York, Marekani wakiomba kuachiwa huru mateka wa Israel waliochukuliwa na Hamas.

Soma zaidi: UN: Guterres asikitishwa na mashambulizi ya Israel, Gaza

Akihutubia umati huo wa watu, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Gilad Erdan, alimkosowa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, kwa kuweka msisitizo kwenye misaada ya kibinaadamu kwa watu wa Gaza badala ya kuachiwa huru kwa mateka.

"Marafiki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atatembelea kivuko cha Rafah huko Gaza. Hivi sasa, cha kusikitisha,  inaonekana kwamba kipaumbele chake kikuu ni kutoa misaada kwa magaidi, magaidi waliowateka nyara wapendwa wetu. Aibu kwake." Alisema Erdan.

Soma zaidi: UN yaomba ahadi mpya kwa ajili ya UNRWA

Akiwa mjini Cairo nchini Misri kutazama maandalizi ya msaada utakaopelekwa kwa Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza, Guterres amesema eneo hilo linahitaji msaada wa kutosha na wa kudumu huku akitoa pia wito wa usitishaji mapigano mara moja kwa ajili ya misaada ya kiutu.