Waliouawa mapigano ya Darfur wafikia 200
27 Aprili 2022Khamis Abdallah Abkar, gavana wa jimbo la Darfur Magharibialiliambia shirika la habari la AP kwamba mapigano hayo ya Jumapili (24 Aprili) kwenye mji wa Kreinik yamewajeruhi pia watu wengine 103.
Gavana huyo alisema washambuliaji waliwazidi nguvu walinda usalama kwenye mji huo, ambao walilazimika kurudi nyuma.
Abkar aliyaita mauaji hayo kuwa ni "uhalifu dhidi ya ubinaadamu", akiongeza kuwa takribani mji mzima wa Kreinik umeharibiwa, yakiwemo majengo yenye taasisi muhimu za serikali.
Mapigano hayo yalichochewa ulipizaji kisasi baada ya kuuawa kwa watu wawili wenye asili ya Kiarabu siku ya Alkhamis, ambapo baadaye alfajiri ya Jumapili kundi kubwa la wanamgambo wa Kiarabu, maarufu kwajina la Janjaweed, waliuvamia mji wa Kreinik ulio umbali wa kilomita 80 kutoka mji mkuu wa Darfur Magharibi, Genena.
Machafuko hayo yalisambaa hadi mjini Genena, ambako hospitali kuu ilishambuliwa.
Risasi zilirushwa hadi kwenye idara ya dharura, ambako mfanyakazi mmoja aliuawa.
Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka linasema kuwa lililazimika kuwaokowa baadhi ya wahudumu wa afya kutoka hospitali hiyo.
Mduara wa visasi
Gavana Abkar alisema pia kwamba mapigano ya siku za Alkhamis na Ijumaa yalipelekea vifo vya watu wanane na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa gavana huyo wa Darfur Magharibi, mamlaka zimechukuwa hatua kubwa za kiusalama kuwalinda raia, ambapo jeshi limetuma kikosi chake maalum kwenye jimbo hilo kuungana na polisi ambao tayari wapo mjini Kreinik.
Uhasama kati ya jamii ya Waarabu na watu wa kabila la Masalit ambao si Waarabu ulianza tangu Disemba mwaka jana, pale mzozo kuhusu umiliki mali kwenye soko ulipogeuka mapigano yaliyouwa watu 88.
Mapigano ya sasa, hata hivyo, yamekuja katika wakati ambapo Sudan nzima imo kwenye hali ya wasiwasi kutokana na machafuko yaliyosababishwa na hatua ya jeshi kuchukuwa madaraka kwa nguvu mjini Khartoum.
Mapinduzi hayo ya kijeshi yalihitimisha kipindi cha mpito kuelekea demokrasia baada ya umma kumlazimisha dikteta wa muda mrefu, Omar Al-Bashir, kuondoka madarakani mwezi Aprili 2019.
Udhaifu wa utawala wa kijeshi
Mapigano ya Darfur yamezusha wasiwasi zaidi endapo utawala wa kijeshi unao uwezo wa kuleta amani katika jimbo hilo, ambalo limekuwa likikumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka kadhaa.
Mnamo mwaka 2020, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliondosha kikosi chake cha kulinda amani kwenye jimbo hilo.
Mzozo wa Darfur ulianza hasa mwaka 2003 pale raia wenye asili ya Kiafrika walipoanzisha uasi, wakiituhumu serikali kuu ya Khartoum inayotawaliwa na Wasudan wenye asili ya Kiarabu kwa kuwabaguwa.
Serikali ya Al-Bashir, ambaye kwa sasa anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilituhumiwa kwa kulipiza kisasi uasi huo kwa kuyapa silaha makabila ya Kiarabu, ambayo yaliunda wanamgambo wa Janjaweed, walioangamiza maelfu ya watu.