1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouwawa shambulio la Al-shabaab Mogadishu wafikia 37

Angela Mdungu
4 Agosti 2024

Waziri wa Afya wa Somalia Ali Haji Adam amesema kuwa idadi ya waliouwawa baada ya mshambuliaji wa kujitoa muhanga na watu wenye silaha kuuvamia ufukwe wenye shughuli nyingi mjini Mogadishu imefikia watu 37

Mashambulizi ya kigaidi yanaiandama Mogadishu
Gari la kubeba wagonjwa likibeba mwili wa mwanamke mmoja aliyeuwawa baada ya mlipuko katika Ufukwe wa Lido, MogadishuPicha: Feisal Omar/REUTERS

Waziri Haji Adam, aliitoa taarifa hiyo Jumamosi usiku kuhusu moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika taifa hilo la mashariki mwa Afrika

Kundi la wanamgambo la Al-Shabaab lilichapisha kupitia tovuti yake na kukiri kuwa ndilo lililohusika na mashambulizo hayo. Mkasa huo, ulianza Ijumaa jioni baada ya mshambuliaji wa kujitoa muhanga kujilipua na kisha watu wenye silaha wakalivamia eneo hilo la ufukwe.

Picha za video zilizochapishwa mitandaoni mara tu baada ya tukio, ziliionesha miili ya watu iliyojawa na damu ikiwa kwenye mchanga.

Kwa mujibu wa waziri wa Afya wa Somalia, majeruhi 11 wa mkasa hicho wako katika vyumba vya wagonjwa mahututi. Wengine 64 wanaendelea kupatiwa matibabu hospitali. Alisema kuwa watu 137 waliopata majeraha madogo waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu. 

Katika shambulio hilo maafisa wa polisi walifanikiwa kuwauwa wanamgambo watano. Al-Shabaab, lenye mafungamano na Al-Qaeda limekuwa likifanya uasi dhidi ya serikali ya Somalia inayotambuliwa  kimataifa kwa zaidi ya miaka 17.

Soma zaidi: Raia wa Somalia waombwa kuungana dhidi ya Al shabaab

Kwa mujibu wa mashuhuda, kulikuwa na umati mkubwa wakati wa tukio hilo, Omar Elmi alisimulia kuwa, "Wakati tulipokuwa tukifurahia ufukweni, mshambuliani wa kujitoa muhanga alijilipua katikati ya umati uliokuwa ufukweni, kisha tuliona watu wengi wakiwa chini wakiwemo waliokufa, majeruhi na wale waliopata mshtuko".

Hawo Mohamed anayeishi karibu na eneo la tukio amesema watu wasiopungua saba aliowafahamu nao waliuwawa. "Uharibifu ni mkubwa na kuna damu na vipande vya nyama za binadamu vilivyotapakaa katika eneo la tukio," Mohamed alisema.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh MohamudPicha: REUTERS

Kufuatia mkasa huo, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kupitia jukwaa la X alitangaza kuitisha mkutano wa dharura na Waziri Mkuu na maafisa muhimu wa usalama ili kujadili hali.

Kauli za kulaani mashambulizi ya Al-Shabaab na salamu za pole zatolewa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake, Ameyalaani mashambulizi ya Al-Shabaab aliyoyataja kuwa ya kigaidi na kuongeza kuwa shirika lake linasimama na Somalia katika vita vyake dhidi ya mashambulizi ya makundi yenye itikadi kali.

Naye mwenyekiti wa tume ya Umoja wa nchi za Afrika Moussa Faki Mahamat, ametoa salamu za rambirambi kutokana na vifo vilivyosababishwa na mashambulizi hayo huku akilaani vitendo hivyo. Kauli ya Wizara ya mambo ya kigeni ya Saudi Arabia nayo imetolewa kuyalaani mauaji hayo na hasa mashambulizi yanayowalenga raia.

Wanamgambo wa Al-Shabaab wamewahi kukiri kuhusika na milipuko na mashambulizi kadhaa Mogadishu na sehemu nyingine za Somalia ambayo serikali yake inapambana na makundi yenye itikadi kali za Kiislamu.

Moja ya hoteli iliyowahi kushambuliwa Mogadishu na kundi la Al Shabaab Agosti 20 2022Picha: REUTERS

Soma zaidi: Al-Shabaab yashambulia kambi za jeshi Somalia na kuwaua watu 25

Eneo la Ufukwe la Lido limekuwa likilengwa katika mashambulizi ya kipindi cha nyuma likiwemo tukio la mwaka 2023 ambalo wanamgambo wa Al-shabaab walizunguka hoteli moja karibu na ufukwe na kuwauwa raia sita. Kando ya mauaji hayo, watu 20 walijeruhiwa.

Mwezi uliopita, watu watano waliuwawa baada ya mlipuko mkubwa wa bomu kutokea kwenye mgahawa mjini Mogadishu. Mwezi Machi, wanamgambo waliwauwa watu watatu na 27 walijeruhiwa baada ya kuizingira hoteli nyingine Mogadishu