1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani waamua

8 Novemba 2016

Dunia nzima leo inaelekeza macho yake Marekani ambapo wapiga kura wataamua iwapo watamchagua rais wa kwanza mwanamke nchini humo, Hillary Clinton, au bilionea maarufu, Donald Trump kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

US TV Debatte Trump vs Clinton
Picha: Reuters/R. Wilking


Wawaniaji hao wawili Hillary Clinton wa chama cha Democratic na mpinzani wake Donald Trump waliendeleza kampeini zao za kipindi cha lala salama hadi saa za alfajiri za siku ya uchaguzi huku waking’ang’ana kuuza sera zao mbali mbali kuhusu mustakabali wa nchi hiyo yenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.
Hillary Clinton wa umri wa miaka 69 aliyepata uungwaji mkono wa wasanii mbalimbali pamoja na rais wa sasa Barack Obama, aliwahimiza raia wa nchi hiyo kuungana na kuchagua serikali itakayowashirikisha watu wote  na yenye matumaini ya baadaye. 
Wakati huo huo, Trump alipeleka kampeini zake kwa wapiga kura wanaojihisi kuachwa nyuma kimaendeleo na kutamatisha kampeini yake kwa msemo, "Marekani kwanza“. Trump aliwaambia wapiga kura hao kutafakari jinsi nchi hiyo inavyoweza kupata ufanisi iwapo raia wataanza kushirikiana na kuwa kitu kimoja chini ya Mungu mmoja na kuheshimu bendera moja. 

Upigaji kura unavyoendelea 
Tayari wapiga kura milioni 40 wamekwisha piga kura katika majimbo yanayoruhusu upigaji kura wa mapema na kura za maoni zinaonyesha kuwa Clinton anaoongoza kwa kiwango kidogo. Kijiji kidogo cha Dixville Notch katika jimbo la New Hampshire ndicho kimekuwa cha kwanza kupiga kura siku ya leo.
Hata hivyo utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la RealClear uilimpa Clinton ushindi wa wastan wa asilimia 3.3 katika uongozi wa taifa lakini Trump anamfuatilia kwa karibu na ana uwezo wa kugeuza mambo kwa kupata ushindi katika majimbo yanayoshikilia turufu ya kuamua mshindi katika kinyang'anyiro cha urais.
Lakini hakuna matokeo yoyote ya uchaguzi yatakayotolewa kabla ya vituo vya kura kuanza kufungwa mwendo wa saa moja za usiku za Marekani hii ikiwa ni saa tisa alfajiri katika saa za Afrika Mashariki.


Mwandishi: Tatu Karema/ AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW