Wamarekani wateremka vituoni kumchagua rais mpya
8 Novemba 2016Siku hii ya leo,inakamilisha kampeni ya muda mrefu ya uchaguzi,iliyozongwa na malumbano ya karaha ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Ulimwengu mzima unasubiri kwa hamu kujua nani atashinda kati ya wagombea hao wawili wakuu wenye mitazamo inayotofautiana kuhusu mustakbal wa dola hilo lenye nguvu zaidi ulimwenguni.
Jina la mshindi halitajulikana kabla ya kesho saa 11 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki. Mgombea mwenza wa Hillary Clinton,ambae pia anawania nafasi ya makamo wa rais Tim Kaine na mkewe Anne Holton walikuwa miongoni mwa wa mwanzo kupiga kura katika ngome yake ya Richmond-Virginia.
Hillary Clinton pia amepiga kura mapema katika kituo chake cha karibu na New York.
Nae mpinzani wake Donlad Trump anatazamiwa kupiga kura wakati wowote kutoka sasa.
Sawa na Kaine wapiga kura kadhaa wametekeleza wajibu wao asubuhi mapema kabla ya kwenda kazini. Katika kituo cha uchaguzi cha Palmetto Bay,kusini mwa Miami-katika jimbo la Florida,mojawapo ya majimbo muhimu katika uchaguzi huu mkuu,watu zaidi ya 20 walipiga kura mara baada ya kituo kufunguliwa.
Katika kijiji kidogo cha Clifton katika jimbo jengine muhimu la Virginia,watu150 walianza kupiga foleni tangu saa kumi na moja na nusu za asubuhi-tokeo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika eneo hilo-wanasema wasimamizi wa uchaguzi.
Zaidi ya wamarekani milioni 42 kati ya zaidi ya milioni 200 walioandikishwa katika orodha za uchaguzi wamepiga kura mapema ili kuepukana na mikururo ya wanaosubiri kutoa sauti zao.
Trump anategea kilichotokea katika kura ya maoni ya Brexit
Ikiwa Hillary Clinton anasemekana anaongoza kwa baadhi ya pointi,hata hivyo Donald Trump pia anasemekana anaweza kushinda.Trump anataraji kuzusha maajabu kama yale yaliyoshuhudiwa katika kura ya maoni ya Uingereza kujitoa katika Umoja wea Ulaya-Brexit.
Mwanawe Eric Trump amesema hivi punde,babaake ataridhia akishindwa kama matokeo yatakuwa ya "haki."Akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni,mtoto huyo wa kiume wa Donald Trump amesema wanachokitaka ni "mashindano ya haki,na sio tu kwa uchaguzi huu bali kwa yote mengine".
Wamarekani wanawachagua pia masenetor 34 na wawakilishi wao
Itafaa kukumbusha hapa kwamba wezani wa nguvu katika bunge la Marekani Congress unaweza kubadilika pia. Wamerakani wanawachagua wajumbe 34 kati ya 100 wa baraza la seneti na pia wajumbe 435 wa baraza la wawakailishi. Wademocrats wanataraji kulidhibiti baraza la Seneti linalomilikiwa hivi sasa na warepublican,sawa na baraza la wawakilishi. Majimbo 12 kati ya 50 yanawachagua magavana wepya,tukitenga idadi kadhaa ya kura za maoni zinazoitishwa kuhusiana na masuala tangu ya kuhalalishwa madawa ya kulevya ya Marijuana hadi kufikia kufutiliwa mbali adhabu ya kifo .
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AP/Reuters/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel