Wamarekani wengi hawaungi mkono vita vya Afghanistan
19 Agosti 2021Kulingana na kura ya maoni ya shirika la habari la AP, kitengo cha utafiti wa masuala ya umma, ni kuwa theluthi mbili ya Wamarekani wanaamini kuwa vita vya miaka 20 vya Marekani nchini Afghanistan havikuwa na maana yoyote.
Kura hiyo ya maoni pia inaonyesha asilimia 47 ya Wamarekani wakiunga mkono jinsi utawala wa Biden unavyosimamia masuala ya kimataifa wakati asilimia 52 wakiunga mkono sera juu ya usalama wa kitaifa.
Kura hiyo ilifanyika kati ya Agosti 12 hadi 16 mwaka huu, baada ya kukamilika kwa vita vya miongo miwili nchini Afghanistan kwa kundi la Taliban kuchukua madaraka. Rais Joe Biden amekosolewa vikali kwa kuanzisha mgogoro wa kibinadamu kwa kuviondoka vikosi vya usalama bila ya mpango maalum.
Soma zaidi: Rais Ashraf Ghani aikimbia Afghanistan
Rais Biden hata hivyo, amesimama kidete juu ya msimamo wake wa kuondoa vikosi vya usalama vya Marekani, akisema hawezi kukubali kuendelea na vita hivyo akiamini kuwa Wamarekani watamuunga mkono.
"Kwa vyovyote vile, hali ya mambo ya nchini Afghanistan inaonyesha wazi kwamba kuondoa wanajeshi wa Marekani ulikuwa uamuzi sahihi."
Wakati hayo yakiarifiwa, waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera za Afghanistan wamemiminika katika miji kadhaa ya nchi hiyo kupinga utawala wa Taliban, katika siku ambayo wanamgambo hao walisherehekea siku ya uhuru wa Afghanistan kwa kutangaza kuishinda Marekani.
Mashuhuda wamesema watu kadhaa wameuawa baada ya wapiganaji wa Taliban kuufyatulia risasi umati wa watu katika mji wa mashariki wa Asadabad.
Taliban yataka maimamu kuwashawishi watu kusalia nchini humo
Licha ya maandamano hayo kuwa madogo, yakijumuisha na idadi kubwa ya Waafghani wanaojaribu kuikimbia nchi, yanaonyesha taswira ya changamoto zinazoikabili Taliban katika utawala wake.
Hii leo kundi hilo limewaomba ma imaam kote nchini humo kujaribu kukabiliana na ripoti hasi kuhusu vuguvugu hilo na kuwashawishi watu kutojaribu kuikimbia nchi, watakapokuwa wanatoa mawaidha katika swala ya Ijumaa hapo kesho.
Soma zaidi: Kwanini Wapakistan wanaliunga mkono kundi la Taliban?
Katika ujumbe wa vidio ulioyotolewa leo wakati makundi ya watu yakiendelea kusubiri nje ya uwanja wa ndege wa Kabul, kupata fursa ya kupanda ndege kuondoka nchini humo, Taliban imesema inatumai ma imaam mjini Kabul na mikoa mingine watazungumzia manufaa ya mfumo wa utawala wa Kiislamu na kuhimiza umoja.
Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema nchi hiyo iko tayari kutoa ndege zake ili kuwahamisha raia wake kutoka Afghanistan wakati dazeni ya Waafghani wakisubiri katika uwanja wa ndege wa Dubai wa Al-Maktoum, kuabiri ndege ya kuwapeleka Uingereza.