Wamisri wajitokeza tena kumuunga mkono Mursi
19 Julai 2013Ndege na helikopta za kijeshi zilionekana juu ya anga ya Cairo tangu kumalizika kwa sala ya Ijumaa, mchana wa leo, kwa kile kinachoonekana kama "kuonesha nguvu za jeshi", ambalo lilimpindua Mursi hapo tarehe 3 Julai.
Mandhari za miji kadhaa ya Misri ilikuwa inasomeka kwa picha za Mursi mbele ya bendera ya Misri, huku watu wakiimba "Kwa pamoja, tutaulinda uhalali!"
Maandamano ya leo yameitwa "kelele za Misri nzima", ambapo kwa uchache majimbo saba yalijaza watu mitaani kumuunga mkono Mursi, yakiwemo ya Alexandria na Ismailiya.
Nje ya msikiti wa mji wa al-Nasr, mjini Cairo, maelfu ya wafuasi wa Mursi walipiga mayowe ya kumlaani mkuu wa majeshi, Jenerali Abdel-Fattah al-Sisi, na kuapa kwamba watamuangusha.
"Umoja wa Kutetea Uhalali" wafanikiwa
Ripoti zinasema muungano wa makundi yanayojiita "Umoja wa Kutetea Uhalali", unaoujumuisha Udugu wa Kiislamu, umefanikiwa kuwashawishi watu wengi zaidi kuhudhuria maandamano hayo kuliko vile ilivyotegemewa na kuliko wapinzani wao wa makundi yanayoitwa ya kiliberali, ambao wameyaita maandamano yao "upinzani dhidi ya magaidi", wakimaanisha Udugu wa Kiislamu.
Vyanzo vya usalama vimesema makabiliano yalizuka kidogo mbele ya msikiti wa chuo kikuu cha al-Azhar, baada ya waandamanaji kuanza kumtukana Jenerali al-Sisi.
Polisi ilirusha risasi hewani kuwachawanya waandamanaji na kuwakamata wafuasi wawili wa Udugu wa Kiislamu, baada ya kuwapiga wapinzani wao kwa fimbo na mawe, kwa mujibu wa polisi. Hata hivyo, hakuna taarifa za watu waliopoteza maisha.
Uingereza yafuta vibali vya silaha
Hayo yakiendelea, Uingereza imetangaza kuzifuta leseni tano za kupeleka silaha nchini Misri.
Waziri wa Biashara wa Uingereza, Vince Cable, amesema hivi leo kwamba hata kama serikali yake haina ushahidi wa silaha za Uingereza kutumika kwenye mashambulizi dhidi ya raia, lakini kwa namna hali ilivyobadilika, imezizuia leseni za kampuni hizo tano kama hatua ya tahadhari, kutokana na ushauri wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Haijafahamika leseni hizo zilikuwa za kampuni gani au za kuingiza silaha za aina gani, lakini kwa sasa Uingereza imo kwenye uhakiki wa leseni za silaha, kuhakikisha kuwa silaha zake hazitumiki kuwashambulia raia wa mataifa yanayouziwa.
Wiki iliyopita, jeshi la Misri liliwauwa waandamanaji 51 wanaoumuunga mkono Mursi, mbele ya makao makuu ya jeshi hilo, kwa kile ilichokiita "kujilinda."
Israel yapeleka makombora ya silaha mpakani
Nayo Israel imetangaza kutuma mitambo yake ya kujilinda na makombora karibu na Bahari ya Sham hivi leo, kutokana na hali inavyoendelea nchini Misri.
Msemaji wa jeshi la Israel ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba mitambo hiyo imepelekwa eneo la Eilat, linalopakana na jangwa la Sinai, ambalo kwa siku za karibuni limeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vyombo vya usalama vya Misri.
Vyombo vya habari nchini Israel vinasema kupelekwa huko kwa mitambo ya kijeshi kunahusiana na vita vya jeshi la Israel dhidi ya wanamgambo kwenye jangwa la Sinai. Shirika la habari la Misri, MENA, liliripoti hapo jana kwamba wanamgambo 10 waliuawa ndani ya siku mbili zilizopita kufuatia operesheni ya kijeshi kwenye eneo hillo.
Hata baada ya zaidi ya wiki mbili za kung'olewa kwa Mursi, bado hakuna ishara ya kufikiwa muafaka wowote wa kisiasa kati ya jeshi na kundi la Udugu wa Kiislamu, na wala hakuna dalili kwamba kundi hilo litarudi nyuma kwenye madai yake ya kutaka, kwanza, Mursi arejeshwe madarakani.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Saumu Yusuf