1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamyanmar wakimbilia India kufuatia vurugu za jeshi

22 Septemba 2021

Wapiganaji wapambana na jeshi la Myanmar katika jimbo la Chin,na kuwafanya mamia kukimbilia vijiji vya India

Myanmar | Unruhen in Magway
Picha: AFP

Watu wengi waliokuwa wakiishi katika mji unaoitwa Thantlang kwenye jimbo la Chin huko Myanmar wamekimbia makaazi yao baada ya nyumba zao kuteketezwa kutokana na makombora yanayorushwa na wanajeshi katika mapambano yanayoendelea kati ya vikosi vya wanamgambo wanaopinga utawala wa kijeshi na wanajeshi wa nchi hiyo.

Takriban watu 10,000 walikuwa wakiishi kwenye mji huo wa Thantlang lakini wengi hivi sasa wameukimbia mji huo kwenda kutafuta hifadhi kwingineko katika maeneo ya karibu ikiwemo wengine kukimbilia India.

Aliyeyaeleza hayo ni msemaji wa jamii ya watu wa mji huo wa Thantlang,mji ulioko kwenye jimbo la Chin  karibu na mpaka wa India. Inaelezwa kwamba wakati vilipozuka vita hivyo kati ya vikosi vya wanamgambo na jeshi la Myanmar mwishoni mwa wiki iliyopita,kiasi nyuma 20 ziliteketezwa huku picha zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha namna majengo yanavyoteketea kwa moto.

Picha: AFP

Kituo kimoja cha habari kinachoitwa Myanmar Now-kiliripoti kwamba wanajeshi walimpiga risasi na kumuua kasisi aliyekuwa akijaribu kuuzima moto huo japo  vyombo vya habari vya serikali viliikanusha ripoti hiyo.

The Global New Light of Myanmar,hili ni gazeti linalomilikiwa na serikali lilisema kwamba kifo cha kasisi huyo kinachunguzwa na kwamba wanajeshi walivamiwa na kiasi watu 100 ambao gazeti hilo liliwaita ni magaidi  na hapo ndipo ulipoanza ufyetulianaji risasi.

Myanmar ni nchi ambayo iko kwenye mgogoro mkubwa tangu serikali iliyokuwa ikiongozwa na mkongwe,mpigania demokrasia  Aung Sang Suu Kyi ilipong'olewa kwa nguvu madarakani na jeshi Februari mosi na kusababisha ghadhabu kubwa nchi nzima,ikashuhudiwa migomo,maandamano na kuzuka harakati  za wanamgambo wanaoupinga utawala huo wa kijeshi.

Kiongozi wa kijamii Salai Thang anasema mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba wapiganaji wa kundi la wanamgambo waliivamia kambi ya jeshi na jeshi nalo likajibu kwa kufanya mashambulizi ya anga.

Salai Thang anasema watu wanne waliuwawa na wengine 15 walijeruhiwa katika wiki za hivi karibuni.

Kikosi cha wanamgambo katika jimbo la Chin wanaojiita,jeshi la ulinzi la Chin,ambacho kinalipinga jeshi la Myanmar kimesema kupitia taarifa yake kwamba  wanajeshi 30 wameuwawa.

Ingawa shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha binafsi juu ya madai yaliyotolewa lakini pia msemaji wa jeshi la Myanmar hakupokea simu wakati akitafutwa kutoa tamko.

Picha: AFP

Mtu mmoja ambaye ni jamaa wa padri aliyeuwawa aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu wengi wameukimbia mji huo wa Thantlang ingawa ziko familia chache zilizobakia ikiwemo watoto 20 wanaoishi kwenye nyumba ya kulea yatima iliyokuwa ikisimamiwa na padiri huyo. 

Thomas Andrews, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Myanmar kupitia ujumbe wa Twitta amekizungumzia kisa cha kuuliwa padiri huyo na nyumba kuchomwa, akisema ni mifano  ya hivi karibuni inayoonesha namna jeshi la Myanmar linavyofanya ukatili dhidi ya watu  nchini humo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Rashid Chilumba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW