1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wana sayansi waishutumu ExxonMobil

Mohammed Abdul-Rahman17 Januari 2007

wasema imeendesha kampeni kupotosha ukweli juu ya ongezeko la ujoto duniani linalosababishwa na gesi zinazochafua mazingira.

Ripoti mpya ya umoja wa wana sayansi wenye wasi wasi, wenye makao yake makuu nchini Marekani, ni kwamba kama vilivyofanya viwanda vya tumbaku ambavyo kwa miongo kadhaa vilikana kuwepo mafungamano kati ya uvutaji sigara na ugonjwa wa kansa, kampuni kubwa ya mafuta ExxonMobil imeendesha kampeni kabambe na ya mafanikio kupotosha ukweli na kuupotesha umma juu ya ongezeko la ujoto duniani.

Ripoti hiyo ambayo inagusia juu ya madai sawa na hayo yaliofanywa na Jumuiya ya Ufalme nchini Uingereza mwezi Septemba, imegundua kwamba kampuni hiyo kubwa ya kibiashara duniani, ilichangia karibu dola 16 milioni baina ya 1998 na 2005, kwa mtandao wa makundi 43 ili kuhoji juu ya ongezeko la kuweko kwa maridhiano madhubuti kwamba utoaji wa gesi za sumu zinazo athiri mazingira, kweli huchangia katika kuongezeka ujoto duniani.

Miongoni mwa wapokeaji wakubwa zaidi wa fedha hizo ni taasisi ya viwanda nchini Marekani American Enterprise Institute, ambapo ExxonMobil iliipatia zaidi ya dola milioni 1 na laki 6, taasisi ya George C. Marshall dola 630,000 na Competitive Enterprise Institute ambayo ilinufaika kwa zaidi ya dola milioni mbili, kiwango kikubwa kuliko nyengine yoyote.

Yakiwa na mabadiliko ya kila wakati ya wakurugenzi, washauri na watumishi wake, makundi hayo 43 kwa mujibu wa ripoti ya umoja huo wa wanasayansi, yaligeuka kama wapiga debe, na kwa msaada wa vyombo vya habari vinavyoelemera siasa za bawa la kulia, kama Wall Street Journal na waandishi wa makala maalum, kusambaza makusudi taarifa zinazopotosha juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti ya kurasa 63 iliopewa jina „Moshi, viyoo na hewa ya moto“, limelitaka bunge jipya la Marekani linalodhibitiwa na Wademokrati, kuitisha uchunguzi juu ya madai ya kampeni ya upotoshaji inayoendeshwa na kampuni hiyo ya ExxonMobil, kama lilivyofanya bunge lililopita dhidi ya kampuni za sigara, kuhusiana na juhudi za kujaribu kuzuwia sheria za serikali kuhusu uvutaji sigara.

Exxon Mobil nalo sasa linajaribu kupotosha ukweli kuhusu athari za ujoto duniani kwa binaadamu, sawa na makampuni ya sigara yalivyofanya kujaribu kukana kwamba uvutaji sigara hausababishi kansa ya mapafu.

Ripoti mpya imetolewa huku kukiwa na ishara kwamba umma wa Marekani na vyombo vikubwa vya habari vikizidi kuwa na wasi wasi juu ya kuongezeka kwa ujoto duniani na kwamba ushindi wa wademokrati katika uchaguzi wa Novemba umebadili nguvu za madaraka katika bunge jipya la Marekani, kwa kuwaunga mkono wabunge wanaounga mkono sheria ya kupunguza au kuwekwa kiwango maalum kinachoruhusu utoaji wa gesi zinazochafua mazingira na kusababisha ongezeko la ujoto duniani.

ExxonMobil , kampuni kubwa kabisa la nishati duniani, limekua kwa muda mrefu likilengwa na wanaharakati walinzi wa mazingira, hasa tangu 1998, kutokana na kuidhinishwa na mataifa meng ya viwanda, kwa ule waraka wa Kyoto kuhusu kupunguzwa viwango vya gesi zinazosababisha ongezeko la ujoto, huku makampuni mengine makubwa hasimu hasa Shell na BP yakianza kujitoa katika ule muungano wa Global Climate Coalition, ambao ni wa mashirika yanayoendesha kampeni kuupinga waraka wa Kyoto.

Kwa uchambuzi wa ripoti , ni kwamba ni dhahiri hii leo kuwa utoaji wa gesi zinazochafua mazingira na, ni moja wapo ya vyanzo vya kuongezeka kwa ujoto duniani.