Wanachama wa ICC warekebisha baadhi ya sheria zake
28 Novemba 2013Marekebisho hayo pia yatakubali viongozi wanaoshikilia nyadhifa za juu kutohudhuria baadhi ya vikao katika mahakama hiyo. Hatua hii inasemekana kumlenga rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye kesi dhidi yake katika mahakama hiyo ya ICC inatarajiwa kuanza rasmi Februari mwaka ujao.
Mahakama hiyo iliyo na wanachama 122 ilifikia uamuzi huo katika mkutano wake wa kila mwaka, uliofanyika katika makao yake makuu, mjini The Hague, Uholanzi.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea mapigano katika ghasia za baada ya uchaguzi nchini humo mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuwawa. Hata hivyo Rais Kenyatta anaendelea kusisitiza kwamba hana hatia. Sasa inasubiriwa kuonekana athari itakayoletwa na uamu huo wa mataifa wanachama wa ICC.
Katika siku za nyuma, majaji wa mahakama ya ICC waliwahi kumuachia Naibu Rais William Ruto, anayeshitakiwa kwa kesi sawa na Rais Kenyatta, ya kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi, aendelee kuwepo nchini Kenya kwa baadhi ya kesi zake ili aweze kutimiza wajibu wake serikalini.
Marekani yaridhia mabadiliko
Mabadiliko yaliofanywa hapo jana yanaweza kuwa na maana kwa kwa washitakiwa waliojitolea kushirikiana na mahakama hiyo kama Uhuru na Ruto kuliko wale walioshikiliwa kwa nguvu na kuwekwa rumande.
Kwa upande wake Marekani ambaye sio mwanachama wa ICC imeyakaribisha mabadiliko hayo na kusema kwamba ICC inapambana na kesi ngumu kwa kuwa inajitayarisha kumshtaki rais ambaye yuko madarakani.
Samantha Power, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema uamuzi huo umewekwa katika hali ya kwamba unalinda haki ya washtakiwa na waathiriwa, huku ukitoa nafasi ya kesi hiyo kuendelea bila kupoteza wakati.
Rais Uhuru Kenyatta, makamu wake Wiiliam Ruto na mtangazaji wa Radio Moja nchini humo Joshua Arap Sang wote wanakabiliwa na mashtaka katika mahakama hiyo ya ICC.
Kenya yataka viongozi wanaoshtakiwa kupewa msamaha
Kenya imekuwa ikijihusisha na mipango ya kidiplomasia ya kusimamisha kwa muda kesi ya Uhuru na Ruto huku ikisema kuwa nchi hiyo na eneo la Afrika ya Mashariki kwa jumla linahitaji uongozi thabiti katika kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab katika nchi jirani ya Somalia.
Kundi hilo la Al shabaab linalosemekana kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed, alisema nchi yake iko mbioni kujaribu kupata msamaha wa mahakama ya ICC kwa viongozi wake kutoshtakiwa wakiwa madarakani.
Thuluthi mbili ya wanachma 122 wa mahakama ya ICC wanapaswa kupigia kura uamuzi kama huo wa kubadilisha Mkataba wa Rome ulioiunda Mahakama hiyo na utaingia katika utekelezwaji mwaka mmoja baada ya sehemu kubwa ya nchi wanachama kuuridhia.
Hata hivyo katika hali nyengine iliojitokeza ni kwamba balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa Macharia Kamau amesema wanachokitaka wao sio kutumika kwa mfumo wa video katika kesi ila kuondoa kabisa mashtaka kwa viongozi walioko madarakani.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP
Mhariri: Mohammed Khelef