1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaahidi kuendelea kusimama na Ukraine

28 Novemba 2023

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO zimeahidi kuendelea kuisaidia Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi. Mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wanakutana mjini Brussels kujadili uungwaji mkono wao kwa Ukraine

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Mkuu wa NATO Jens Stoltneberg amewahimiza wanachama kuendelea kusimama na UkrainePicha: Government of North Macedonia

Akizungumza wakati akiwasili Jumanne mjini Brussels kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO katika makao makuu ya jumuiya hiyo, katibu mkuu wa muungano huo wa kijeshi Stoltenberg amesema ni wajibu wao kuhakikisha kuwa wanaipa Ukraine silaha inazohitaji.

Soma pia: Mkuu wa NATO asema vita vya Ukraine vitachukua muda mrefu

Itakuwa ni janga kwa wananchi wa Ukraine iwapo rais Putin atashinda, lakini pia itakuwa hatari kwetukwa sababu itatuma ujumbe kwa viongozi wote wa kimabavu, si kwa Moscow pekee, bali pia kwa wale wa Beijing, kuwa wanapokiuka sheria za kimataifa, wanapovamia nchi nyingine, wanapotumia mabavu wanapata wanachokitaka.

Matamshi yake yanajiri huku hatima ya mpango wa msaada wa kijeshi wa Marekani wa thamani ya dola bilioni 60 uliopendekezwa na utawala wa Biden ikiwa katika hali ya sintofahamu kutokana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wabunge wa Republican.

Mshikamano kwa Ukraine waendelea 

Marekani imetoa msaada wa kijeshi wa zaidi ya dola bilioni 40 kwa Ukraine tangu uvamizi wa Urusi na kuahidi kuiunga mkono kwa muda wote itakaouhitaji.

Maafisa wa serikali wameelezea imani kuwa watauidhinisha mpango huo, wakisema wengi wa Warepublican na Wademocrat katika Bunge la Congress bado wanaiunga mkono Kyiv. Stoltenberg pia ameonyesha matumaini.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken alisema mawaziri wenzake watasititiza uungwaji mkono wao kwa Ukraine wakati inaendelea kukabiliwa na vita vya uchokozi vya Urusi.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya kwa sasa pia unapata ugumu kukubaliana kuhusu mpango wa uungwaji mkono wake wa muda mrefu wa kuipa silaha Ukraine licha ya upinzani kutoka kwa Hungary.

Ukraine itashinikiza mpango wa kujiunga na NATOPicha: Thomas Peter/REUTERS

Soma pia:Jumuiya ya Kujihami ya NATO imekuwa ikipita katika nyakati tete katika miaka ya karibuni na hasa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Stoltenberg amewahimiza wachama kuendelea kutoa msaada akisema tayari Ujerumani na Uholanzi ziliahidi hivi karibuni kutoa euro bilioni 10.

Ujerumani: Muhimu ni kuwaokoa Waukraine

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema hitaji la kuiunga mkono Ukraine sio kama Ukraine inaweza kupiga hatua zozote kijeshi, bali ni kuhusu kuwaokoa watu.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Mwenzake wa Ufaransa Catherine Colonna amesema Kyiv inakabiliwa na mashambulizi makali zaidi ya angani tangu kuanza kwa vita hivyo.

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Latvia Krisjanis Karins amesema Ukraine inahitaji makombora ya masafa marefu ili kuzuia uwezo wa usafirishaji wa vifaa vya Urusi.

Soma pia:Ukraine yasema Urusi inaongeza mashambulizi mji wa Avdiivka

Mwanadiplomasia mkuu wa Ukraine Dmytro Kuleba atajiunga na mkutano huo kesho Jumatano na wanachama wa NATO wanatarajiwa kukubaliana kuhusu mpango wa mageuzi yanayolenga kuisaidia Ukraine kuelekea hatimaye kuwa mwanachama wa muungano huo wa kijeshi.

Ukraine inashinikiza kujiunga na NATO, lakini muungano huo unaoongozwa na Marekani mpaka sasa umekataa kutoa mwaliko rasmi licha ya kuahidi kuwa Kyiv itakuwa mmoja wa wanachama wake siku moja.