Wanachama wa SPD waidhinisha ilani ya uchaguzi
26 Juni 2017Chama hicho kinakinataka kuungwa mkono na wapiga kura na kuifikisha mwisho safari ya kansela Angela Merkel kuwapo madarakani kwa muda wa miaka 12 katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Septemba.
Katika mkutano uliokuwa na msisimko mkubwa , kiongozi wa SPD Martin Schulz amemshutumu kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa kuzima mjadala kuhusiana na masuala kama mafao ya uzeeni na kushindwa kusimama imara dhidi ya Marekani.
Chama cha SPD kimepata nguvu kubwa katika maoni ya wapiga kura baada ya Schulz kutangazwa kuwa kiongozi wa chama hicho mwezi Januari mwaka huu, akikipita chama cha kansela Merkel cha CDU, katika baadhi ya mambo, lakini mafanikio hayo yameyeyuka hivi sasa na chama kinahangaika kurejea katika njia yake. Kansela wa zamani Gerhard Schroeder amehamasisha katika mkutano huo kwa kusema inawezekana kubadilisha hali hiyo.
"Iwapo tutakusanya nguvu zetu zote katika wiki chache zijazo na kupambana kutafuta kila kura, tunaweza kufanikiwa kukifanya chama cha SPD kuwa chama kikubwa."
Katika hotuba iliyochukua dakika 80 kabla ya chama hicho kukubaliana na sera zilizomo katika ilani ya uchaguzi, Schulz rais wa zamani wa bunge la Ulaya, alionesha mapenzi makubwa kwa Umoja wa Ulaya.
Kiburi cha madaraka
Merkel na waziri wa fedha Schauble wako imara sana zinapokuja sera kama kubana matumizi kwa mataifa ya Ulaya lakini husikii chochote kutoka kwao juu ya utawala wa sheria na demokrasia katika Umoja wa Ulaya, ameyasema haya akiilenga Hungary na Poland.
Amesema chama cha SPD kinalenga kuimarisha Ulaya na kusisitiza maadili ya utu na kuwekeza katika kuweka hali mpya.
Nafasi ya kumnyima Merkel muhula wa nne inaonekana kuwa finyu kwa SPD, chama ambacho ni mshirika mdogo katika serikali ya muungano wa siasa za wastani za mrengo wa kulia na kushoto, lakini baadhi wametiwa moyo na kile kilichotokea Uingereza ambapo chama cha Labour chini ya Jeremy Corbyn kilibadilisha mambo katika uchaguzi wa hapo Juni 8.
Martin Shulz alimshambulia kansela Merkel kwa kumshutumu kuwa na kiburi katika mambo kadhaa ya uongozi.
Wakati chama kinasema hatuna chochote cha kufanya kuhusu hili na hatuwezi kujadili hili katika kipindi cha kampeni, hii ni kiburi cha madaraka, hakuna kingine, wapenzi mabibi na mabwana."
Kukiwa kumebakia wiki kadhaa kabla ya Ujerumani kuingia katika uchaguzi hapo Septemba 24 , chama cha SPD kiko nyuma ya chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU kwa asilimia 15 ya alama, kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya wapiga kura uliochapishwa jana Jumapili na gazeti la Bild.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Josephat Charo