Wanadiplomasia wa Kiarabu na Ulaya wakutana kuisaidia Syria
12 Januari 2025Wanadiplomasia wakuu kutoka Mashariki ya Kati na Ulaya, wamewasili katika mji mkuu wa Saudi Arabia wa Riyadh leo Jumapili, kwa mazungumzo ya kuisaidia Syria. Mataifa yenye nguvu duniani yanashinikiza kuwepo kwa utulivu baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.
Mazungumzo ya leo yatafanyika katika mikutano miwili, wa kwanza utakutanisha maafisa wa Kiarabu, huku mkutano wa pili ukiwa na ushiriki mkubwa zaidi wa wawakilishi wa Uturuki, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.
Saudi Arabia, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi katika Mashariki ya Kati, inataka kuongeza ushawishi wake nchini Syria baada ya muungano wa waasi ukiongozwa na kundi la itikadi kali la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kumuangusha Assad mwezi uliopita.
Kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa, ambaye aliongoza kundi hilo kumwangusha Assad, anashinikiza taifa hilo kuondolewa vikwazo.