1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wakutana Luxemburg

26 Juni 2023

Suala la uasi wa kundi la mamluki la Urusi la Wagner linatarajiwa kutawala ajenda kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya unaofanyika leo nchini Luxembourg.

Belgien Treffen der EU-Außenminister in Brüssel
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kwenye picha ya pamoja mjini Brussels, Ubelgiji.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Kando na kadhia ya vita vya Ukraine, mkutano huo pia utajadili jinsi ya kushughulikia mizozo inayotokea ndani ya Umoja huo. 

Mwanadiplomasia Mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borell alishauriana na wenzake mwishoni mwa juma juu ya kinachoendelea nchini Urusi, wakati wapiganaji wa Wagner walipoonekana kuelekea Moscow kwa lengo la kuuangusha utawala wa jeshi la Urusi. Hata hivyo, hilo halikutokea.

Soma pia: EU yawaita viongozi wa Serbia na Kosovo kwa mazungumzo

Borrell ambaye ni mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema uasi wa Wagner unaonyesha kuwa vita vya Urusi nchini Ukraine vinasambaratisha nguvu ya Urusi na kuathiri mfumo wake wa kisiasa.

Ameongeza kuwa, ukosefu wa utulivu katika taifa hilo lenye kumiliki silaha za nyuklia, "sio jambo zuri.”

Borrell: Tutaendelea kuiunga mkono Ukraine hadi mwisho

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP/dpa/picture alliance

Borrell ameeleza, "Mnyama wa kutisha ambaye Putin alimuunda, Wagner, sasa anamtafuna mwenyewe. Zimwi limemgeuka. Mfumo wa kisiasa unaonyesha udhaifu wake na nguvu za jeshi zinayumba. Hali hii ina athari ya moja kwa moja kwa vita vya nchini Ukraine."

Wakiungana na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba kwa njia ya video, mawaziri hao wanatarajiwa kusisitiza mshikamano wao na Ukraine na kuja na mipango madhubuti ya kuipa silaha zaidi nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Ukraine inatarajiwa kupokea makombora milioni 1 na wanajeshi wake 24,000 kupata mafunzo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa kauli moja, mawaziri hao pamoja na nchi washirika wameamua kuiongezea Ukraine msaada zaidi wa kijeshi wa dola bilioni 3.82.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Josep Borrell ameandika, "Tutaendelea kuongeza msaada wa kijeshi kwa njia ya silaha na mafunzo.” Kauli iliyoungwa mkono na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.

Ajenda nyengine zinazotarajiwa kuwepo kwenye meza ya mazungumzo huko Luxembourg ni mvutano unaoongezeka kati ya Kosovo na Serbia, mzozo kati ya Armenia na Azerbaijan na suala la wakimbizi nchini Tunisia.

Soma pia: Mpango wa EU wa kuokoa uchumi wa Tunisia

Ama kuhusu mvutano kati ya Kosovo na Serbia, juhudi za upatanishi za hivi karibuni zilizofanyika wakati wa mkutano wa Brussels zilileta maendeleo madogo juu ya suala hilo.

Umoja wa Ulaya unafikiria kuipa Tunisia msaada wa kifedha wa hadi euro milioni 980, wakati huu ambapo nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imetumbukia kwenye matatizo ya kiuchumi na pia inakabiliwa na wimbi la wahamiaji ambao wanaitumia Tunisia kama njia ya kuingia Ulaya.

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa pia kuiwekea Iran vikwazo vipya kutokana na visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyoendelea nchini humo.

Kando na kujadili mizozo, mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya Caribbean na Amerika ya Kusini EU-CELAC pia ni mada ambazo zipo kwenye ajenda yao kuelekea mkutano wa kilele na mataifa hayo uliopangwa kufanyika mjini Brussels mnamo mwezi Julai 17-18.

Vyanzo: dpa/reuters/afp

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW