1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi 279 waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru

2 Machi 2021

Mamia ya wanafunzi wa kike waliokuwa wametekwa nyara Nigeria na makundi ya wahalifu wiki iiyopita, wameachiwa huru. Gavana wa jimbo la Zamfara, Dokta Bello Muhammad Matawalle amesema wanafunzi wote 279 wameachiwa huru.

Nigeria Freilassung entführter Schülerinnen
Picha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Akizungumza na waandishi habari, Matawalle amesema kuwa jana maafisa wa serikali walifanya mazungumzo na watekaji nyara na kwamba hawakuwa na nia ya kupeleka vikosi vya usalama kwa hofu ya kuyaweka hatarini maisha ya wasichana hao. Awali serikali ya Nigeria ilisema wasichana waliotekwa nyara Ijumaa iliyopita kutoka kwenye mabweni yao ni 317, katika shule ya wasichana inayomilikiwa na serikali kwenye kijiji cha Jangebe.

Wasichana wana afya nzuri

Matalle amesema baada ya wasichana hao kuokolewa, walipelekwa kwenye ukumbi wa ofisi ya serikali ya jimbo la Zamfara na wote wana afya njema na wanamshukuru Mungu kwa hilo.

''Leo tumefanikiwa kuwaokoa, wasichana hawa wako nasi. Hatukulipa pesa zozote kwa ajili ya wasichana hao kuachiwa huru, kwa sababu watekaji wenyewe pia wanataka amani. Tutaongeza usalama kwenye eneo hili ili tukio jengine kama hilo lisitokee tena. Inshallah,'' alisema Matawalle.

Hata hivyo, wasichana wengi wanaonekana hawajapata madhara, lakini baadhi yao wamepelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Wasichana hao walikuwa peku na wengine kati yao walikuwa na majeraha miguuni.

Timu ya maafisa wa usalama wakiwa kwenye shule ya Jangebe, ZamfaraPicha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Msemaji wa jimbo la Zamfara, Suleiman Tanau Anka amewaambia waandishi habari kwamba baadhi ya wasichana waliokuwa hawajulikani waliko, walikimbia kwenye msitu wakati wa utekaji nyara huo. Waandishi habari wa Reuters na AFP wamewashuhudia wasichana hao wakiwa wamevalia vazi la Hijab na waliondolewa katika eneo hilo kwa mabasi madogo baada ya baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao kuwasili.

Wazazi wazungumza

Mmoja wa wazazi wa wasichana hao waliotekwa nyara ameelezea namna alivyofurahishwa baada ya kuonana na binti yake. ''Nina furaha sana, siwezi hata kuelezea jinsi nilivyo na furaha leo. Nimemuona binti yangu na ana afya njema,'' alieezea baba huyo ambaye jina lake halikutajwa.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amesema amepokea kwa furaha taarifa za kuachiliwa huru wasichana hao na kwamba anaungana na familia zao na watu wote wa Zamfara kusherehekea ushindi huo. Rais Buhari ametoa wito wa kuwepo umakini zaidi kwa ajili ya kuwazuia wahalifu kufanya mashambulizi mengine kama hayo na ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya watekaji.

Utekaji nyara katika jimbo la Zamfara, ni wa pili kufanyika ndani ya wiki moja katika eneo la kaskazini magharibi mwa Nigeria, eneo ambako vitendo vya makundi ya kihalifu vinaongezeka. Jumamosi iliyopita watu wenye silaha waliwaachia huru wavulana 27 waliokuwa wamewateka nyara kutoka kwenye shule yao Februari 17 kwenye jimbo la Niger.

(AP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW