Wanafunzi 8 wafariki katika ajali mkoani Mtwara, Tanzania
26 Julai 2022Ajali hiyo imetokea majira asubuhi ikihusisha gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili wa T207 CTS ambayo ni mali ya Shule ya Msingi King David hapa mkoani Mtwara.
Kulingana na Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Nicodemus Katembo amesema chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki ambako kulipelekea gari kuacha njia na kuingia kwenye mtaro ulio pembezoni mwa barabara, huku akisema kuwa taarifa zaidi atazitoa hapo baadaye.
Katembo amesema, "Chanzo cha ajali kwa harakaharaka tulivyoona pale ni kwamba kulikuwa na hitlafu kwenye breki, na kwa sababu eneo lenyewe linamteremko basi dereva akashindwa kulimudu na likaingia kwenye mtaro mkubwa uliokuwa pembezoni mwa barabara."
Akizungumzia hali ya majeruhi na vifo Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta Hamad Nyembea amesema miili na majeruhi imepokelewa kwenye hospitali ya rufaa ya ligula na waliofariki kwenye ajali hiyo ni wasichana watano, wavulana watatu na watu wazima wawili ambao ni Dereva wa gari hiyo na mhudumu wa watoto.
"Lakini mpaka sasa tunajumla ya wagonjwa watano ambao hali zao kidogo ziko mahututi, mwingine yuko chumba cha upasuaji na wengine wanaendelea kupatiwa matibabu yale ya ICU ili kuona kama tunaweza kuwasaidia kuwaokoa maisha yao." ameongeza Dokta Hamad.
Majeruhi 19 wamehifadhiwa katika hospitali hiyo huku watano wakitajwa kuwa kwenye hali mbaya zaidi.
Mganga huyo amesema kuwa hospitali hiyo inauwezo wa kuwahudumia manusura wote wa ajali.
Baadhi ya wazazi waliojitokeza kushuhudia majerehi wa ajali hiyo wameelezea hisia zao.
"Wanangu wanasoma King David mmoja yupo bweni na mwengine anaishi nyumbani, lakini nimekuja hapa baada ya kupigiwa simu, nimekuja hapa kusubiri, kuna watu wanafuatilia humo ndani kama salama itakuwa imepita au vipi tutajuwa baadaye, tangu nipate hizi taarifa moyo wangu haujatulia" ameeleza Seif Jamali ambaye ni mmoja wa wazazi wa wanafunzi waliopata ajali.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameelezea kusikitishwa kwake kutokana na ajali hiyo na kutoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto wao ndugu na jamaa, pamoja na mkuu wa mkoa Mtwara.
Katika Salamu zake za rambirambi alizoziandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia amesema; “Nimesikitishwa na vifo vya wanafunzi 8 wa shule ya msingi ya King David na watu wazima wawili vilivyotokea leo asubuhi huko Mtwara Mikindani baada ya gari la shule kutumbukia shimoni. Nawapa pole wafiwa, Mkuu wa Mkoa, Jamaa na ndugu za waliofiwa. Mwenyezi Mungu awarehemu marehemu na kuwaponya majeruhi.”