1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi DRC washinikiza Rais Tshisekedi kuzuru Beni

John Kanyunyu28 Aprili 2021

Mgomo wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopiga kambi kwenye ofisi ya meya mjini Beni, wakishinikza Rais Félix Tshisekedi kwenda Beni kusimamia operesheni za kijeshi waendelea Beni.

Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mgomo wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopiga kambi kwenye ofisi ya meya mjini Beni, wakishinikza Rais Félix Tshisekedi kwenda Beni kusimamia operesheni za kijeshi za kurejesha amani katika eneo hilo umeingia siku yao ya sita Jumatano, huku jeshi likielezea hofu juu ya kutokea kwa shambulizi la waasi wa kundi la ADF dhidi ya wanafunzi hao.

Katika mazungumzo maalumu na DW, kamanda wa operesheni za kijeshi dhidi ya waasi kutoka Uganda ADF pamoja na makundi mengine ya waasi katika wilaya za Beni na Lubero, Meja Jenerali Peter Cirimwami alisema, kwamba taarifa walizo nazo zinabaini, kwamba ADF wanakusudia kuwashambulia wanafunzi hao kwa matamshi hayo.

Marekani yapiga marufuku makundi mawili ya DRC na Msumbiji

Wanafunzi wapuuza vitisho vya ADF

Wanafunzi hao hata hivyo, wamepuuza vitisho vya ADF dhidi yao, na kusema kwamba, ni njama ya viongozi wa kijeshi pamoja na kiraia, ya kuwataka waondoke kwenye ofisi ya Meya, wanakomsubiri rais Félix Tshisekedi, aje kusimamia mwenyewe operesheni za kijeshi dhidi ya ADF.

"Sisi wanafunzi kupitia kikosi chetu cha usalama, tulimshika mtu mmoja anayetajwa kuwa ni maimai na kumkabidhi kwa polisi kwani alijipenyeza katika eneo tunamokaa bila ya kuvaa mavazi ya wanafunzi. Kwa hiyo tunawaomba kutoamini uchambuzi wa viongozi fulani kwani wako tayari kwa lolote lile ilikuhalalisha msimamo wao," amesema mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka kutambulishwa jina.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix Tshisekedi Picha: Giscard Kusema

Usalama Beni umedorora kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara

Kwa siku sita zilizopita, wanafunzi hao wamekuwa wakilala nje. Wamewaambia wanahabari, kwamba wataendelea kulala nje, hadi pale Rais Félix Tshisekedi atakapofika Beni kusikiliza malalamiko yao, ambayo ni kurudisha usalama katika eneo hilo, ambako waasi kutoka Uganda ADF, wamekuwa wakiwaua wakaazi kwa karibu miaka saba sasa.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kuidhinishwa jana jumanne, waziri mkuu wa DRC Sama Lukonde alisema kwamba usalama sio tu kipaumbele kwa serikali yake, bali ni suala la dharura.

Na ilikutimiza ahadi yake kuhusu usalama katika eneo la mashariki ya Congo, huenda wakateuliwa ma ofisa wa jeshi ilikuongoza miji, wilaya pamoja na vijiji mbalimbali, katika eneo hili la mashariki ya Congo, hasa maeneo yanayoshuhudia vita.