1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wanafunzi Kenya huenda wasifanye mitihani ya taifa

Shisia Wasilwa
13 Januari 2022

Maelfu ya wanafunzi katika jimbo la Baringo nchini Kenya, huenda wakakosa kufanya mitihani ya kitaifa iliyoratibiwa kuanza mwezi Machi mwaka huu. Shule kadhaa zimefungwa kutokana na mashambulizi ya wezi wa mifugo.

Kenia Schüler bei Abschlussprüfung für
Picha: DW/Shisia Wasilwa

Watu 60 wameaga dunia kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na uvamizi wa mara kwa mara unaosababisha ukosefu wa usalama. Hali ya taharuki imetanda Baringo Kaskazini na Baringo Kusini baada ya wavamizi kuyavamia maeneo hayo na kuwaiba zaidi ya mifugo 200. Hali ambayo imesababisha kusitishwa kwa masomo katika maeneo hayo.

Shule 10 zimefungwa

Wazazi na wanafunzi wakitorokea maeneo salama. Wavamizi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha wamasebabisha shule kumi kufungwa hadi kufikia sasa. Shule zaidi ya tano zimefungwa Baratabwa huku shule nyingine tano zikifungwa eneo la Mochongoi.

Kulingana na katibu wa chama cha walimu KNUT jimbo la Baringo, Joshua Cheptarus, watahiniwa na mitihani wameathirika pakubwa na serikali inafaa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama shuleni Ili walimu na wanafunzi warejee shuleni, ikizingatiwa kwamba mitihani miwili ya kitaifai inatarajiwa kufanywa mwaka huu.

Moja ya eneo lililochomwa moto katika mapigano ya kikabila katika Bonde la Ufa, KenyaPicha: AP

Viongozi wanazidi kutoa wito kwa serikali kurejesha maafisa wa polisi wa akiba ili kusaidia katika kurejesha amani. Serikali iliwaondoa maafisa hao, huku ikitwaa bunduki walizokuwa nazo kwenye operesheni ya kurejesha amani katika eneo hilo.

Viongozi na wakazi waliandaa maandamano kufuatia visa hivyo vya mashambulizi. Wamehimiza serikali kuingilia kati, kufikia sasa watu zaidi ya 60 wameuawawa bonde la Kerio kwa muda wa miezi miwili. 

Soma zaidi: Watu 11 wauawa kwenye mapigano mapya Kenya

Haya yanajiri siku chache tu baada ya aliyekuwa Mratibu wa Bonde la Ufa George Natembea kuzuru maeneo hayo kubaini hali ya ukosefu wa usalama. Chifu wa kata ya Yatia Jackson Keitany amesema kuwa wavamizi walifanya maasi hayo wakiwa wanaandaa maziko ya Vincent Tuwit, mwenye umri wa miaka 24 na Kipkenei Kimurio mwenye umri wa miaka 65 waliouawa kwenye shambulizi la uvamizi juma lililopita. 

Mwaka uliopita, zaidi ya watu 80 waliuawa huku maelfu ya wengi wakipoteza makazi na mifugo kuibiwa. Wavamizi hao wanatokea majimbo ya Pokot Magharibi, Elgeyo-Marakwet na Baringo. Wakazi wamekuwa wakiiomba serikali kuangazia tatizo lao bila ya mafanikio. Inaaminika kuwa zaidi ya bunduki 6000 ziko mikononi mwa raia katika jimbo la Baringo.