1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi Kenya wachoma shule kabla ya mitihani ya taifa

Wakio Mbogho26 Januari 2021

Wasiwasi umeibuka kuhusu mwenendo wa wanafunzi wa shule za upili nchini Kenya kuchoma majumba na mali ya shule, wiki sita tu kabla ya kufanyika mitihani ya kitaifa

Afrika Coronavirus Pandemie / Kenia
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Ofisi ya mkuu wa upelelezi imetangaza kwamba imewakamata baadhi ya wanafunzi waliohusika wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 inapoendelea kufanya uchunguzi zaidi, nayo wizara ya elimu ikilaani vitendo hivyo na kuapa kuchukua hatua kali.

Ni wiki tatu tangu shule zifunguliwe nchini Kenya baada ya kipindi kigumu cha mapambano na janga la COVID 19, lililowapotezea wanafunzi mwaka mzima wa masomo. Lakini sasa mwenendo unaotia wasiwasi wa wanafunzi kuzua vurugu na kuchoma majumba na mali ya shule, wiki sita kabla ya kufanyika mitihani ya kitaifa unashuhudiwa kwenye shule za upili. Daniel Tarus, mkurugenzi wa elimu wa Bungoma alitangaza kufungwa kwa shule hiyo kwa muda usiojulikana.

"Kama wasimamizi wa bodi wa shule hii, tumeamua kwamba wanafunzi wote wajiandae na waondoke shuleni, tutawasiliana nanyi baadaye,” alisema mkuu wa shule.

Wanafunzi nchini Kenya wamerejea shuleniPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Katika kipindi cha siku mbili pekee, shule tano zikiwemo shule ya upili ya Chesamisi na St Luke huko Bungoma, shule za upili za Kituro na Timboroa huko Baringo na shule ya upili ya Kimulot huko Bomet zimeshuhudia matukio ya kuchomwa kwa mabweni, madirisha kuvunjwa na mali nyingine kuharibiwa. Kwenye baadhi ya visa hivi wanafunzi wanalalamikia kutoruhusiwa muda wa burudani, kuadhibiwa au kubadilishiwa ratiba.

Ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi nchini Kenya imetoa tahadhari kwa wanafunzi wa shule za msingi, upili, vyuo vikuu na taasisi zinginezo kwamba idara hiyo inakusanya na kuweka ushahidi wowote wa kihalifu dhidi ya wanafunzi. Ofisi hiyo inaonya kwamba hii ni taarifa ya kudumu itakayowekwa kwenye rekodi za wanafunzi hao na itawazuia wengi kuzifikia ndoto zao.

Polisi wamewakamata na kuwafungulia mashtaka wanafunzi walio na umri wa kati ya miaka 15-19 wa shule za upili ya Kiambere na Kiritiri huko Embu waliohusika na uchomaji wa mabweni ya shule. Waziri wa elimu George Magoha ametangaza kuwa mwenendo huo kati ya wanafunzi hautovumiliwa.

"Tuwache kuwachukua watoto kama mayai. Unatakikana umruhusu mwanao atayarishwe kukabiliana na maisha. Kama waalimu lazima muwe imara, na mwanafunzi yeyote anayefikiri kwamba kwa sababu yeye ni mtoto anaweza kumshambulia mwalimu au kuzua vurugu, afahamu kwamba tutakabiliana naye. Nawataka waalimu waendelee kuwaadhibu wanafunzi bila uoga.”

Magoha anawakosoa wazazi kwa malezi mabaya akisema hali hii inachangiwa na wazazi kutokubali watoto wao waadhibiwe.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW