Wanafunzi wa Uganda wavumbua "Mafuta-Go"
7 Novemba 2012Edward Sekeywa anaendesha gari lake mjini Kampala. Tangi lake la mafuta linakaribia kuwa tupu na hivyo ni lazima aharakishe kwenda kununua mafuta. Lakini mafuta hayo yanauzwa kwa bei ghali mjini Kampala. Hata hivyo, bei zinatofautiana kutoka kituo kimoja cha mafuta hadi kingine. Ili kufahamu mahali atakapoweza kununua mafuta kwa bei nafuu, Edward anaitazama simu yake ya mkononi.
"App hii inanionyesha mahali ninapoweza kupata mafuta ya bei rahisi zaidi hapa mjini na kituo kilichopo karibu na hapa nilipo. App inafahamu mahali nilipo na hivyo inanionyesha vituo vya mafuta vilivyopo karibu. Nadhani ni jambo la muhimu kwa sababu ya kupanda na kushuka kwa bei katika mtaa huu wa Kololo. Hivi sasa nimechagua kituo cha mafuta kiitwacho City Oil Kamocha na App hii inanionyesha kwamba pale mafuta yanauzwa kwa shilingi 3,350. Nitakwenda kujaribu." Anasema Edward.
Edward Sekeywa anaanza safari. Ana umri wa miaka 40 na ni mmoja wa watu wa tabaka la kati linaloongezeka nchini Uganda. Bw. Sekeywa anafanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali. Anamiliki gari aina ya Volkswagen na nyumba na ana mtoto mmoja tu. Ingawa anapokea mshahara mzuri, Sekeywa anaeleza kwamba ni lazima atumie fedha yake kwa busara. Anapofika kwenye kituo cha mafuta, anashtuka.
"Hili ni jambo la ajabu. App hii ilinionyesha kwamba bei ya mafuta ni shilingi 3,350 lakini hapa bei ni 3,600. Samahani bwana. Hujambo? Mafuta yanauzwa shilingi ngapi? Sawa, basi nitachukua ya shilingi 20,000. Ameniambia kwamba kwa mara ya mwisho walikuwa na bei ya 3,350 wiki moja iliyopita."
"Mafuta-Go"
Mafuta yanauzwa kwa bei ghali Uganda. Ingawa hakuna kodi inayotozwa, mafuta hayo ni lazima yasafirishwe hadi bandari ya Mombasa na kisha kuchukuliwa kwa magari maalum na hatimaye kufikishwa kwenye vituo vya uuzaji. Hivyo, gharama ya usafirishaji ndiyo inayoifanya bei ya mafuta iwe juu.
Hivyo ni muhimu mtu alinganishe bei, kabla ya kulijaza gari lake mafuta. Hilo ni jambo lililogunduliwa mapema na wale walioubuni huduma ya kulinganisha bei za mafuta.
Christine Ampaire na Daniel Odong ni wanafunzi wa teknolojia ya habari. Wanaeleza kwamba mwaka moja uliopita walianzisha kampuni yao walioipa jina la Code-Sync. App yao iitwayo Mafuta-Go ni ya bure na inaweza kutumiwa na kila mtu. Ampaire na Odongo waliweza kugharamia utengenezaji wa App hiyo kwa fedha walizoshinda katika shindano Pivot East la kubuni Apps za simu za mkononi.
Wavumbuzi wa "Mafuta-Go"
Ampaire na Odongo waliweza kujinyakulia zawadi ya dollar za Kimarekani 10,000. Hivi sasa watumiaji wa App ya Mafuta Go wanaweza pia kupata taarifa juu ya mahala panapouzwa mafuta kwa bei rahisi kupitia ujumbe unaotumwa katika mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter.
"Tunajitahidi sana kuwa na ushirikiano na vituo vya mafuta ili programu ya Mafuta Go iweze kujazwa taarifa kutoka vituo hivyo moja kwa moja. Lakini hivi sasa inabidi kila asubuhi tumtume mtu na pikipiki kwenda kuchunguza bei za mafuta katika vituo vya Kampala." Christine Amapire anaelezea mipango yao ya baadaye.
Mbali na kuwaonyesha watu bei mkatika vituo vya mafuta, App ya Mafuta go inamwarifu pia mtumiaji wake iwapo kituo fulani kimeishiwa kabisa mafuta.
Mwandishi: Simone Schlindwein
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman