1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi waandamana Venezuela

Yusra Buwayhid
5 Mei 2017

Mauaji ya mwanafunzi wa miaka 18 katika maandamano ya Venezuela ya kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro, yameifanya idadi ya vifo kuzidi 30. Huku Amerika Kusini ikiitolea wito Venezuela kuheshimu haki za raia wake.

Venezuela Caracas Demonstrationen
Picha: Getty Images/AFP/R. Schemidt

Mwanafunzi huyo aliuliwa na mtu aliyempiga risasi mara kadhaa na baadaye kukimbia kwa kutumia pikipiki. Hata hivyo, haikuwekwa wazi kama tukio hilo linahusika na maandamano ya wanafunzi yaliyokuwa yakiendelea kwa wakati huo.

Makundi ya wanafunzi yalipambana na polisi wa kuzuwia ghasia, waliokuwa wakirusha mabomu ya kutoa machozi, wakati mgogoro huo ukiendelea kupamba moto katika taifa lenye utajiri wa mafuta huku kukiwa na uhaba wa chakula, dawa pamoja na mahitaji mengine ya msingi.

"Huu ni upinzani sio vurugu, tunajua kwamba mapambano hayatomalizika leo, lakini tutastahmili, maandamano haya yana waleta pamoja watu ambao hawaitaki serikali hii, inayowashambulia raia wote wa Venezuela wanaotaka mabadiliko," amesema Rafaela Requesens mmoja wa waandamanaji.

Wapinzani wa rais Maduro wa siasa za mrengo wa kushoto wanamshutumu kwa kujaribu kujiongezea muda kwa kuchelewesha uchaguzi, pamoja na kuzindua mchakato wa kisheria wa kuifanyia mabadailiko katiba ya nchi.

Katika ujanja wake wa hivi karibuni wa kujaribu kudhibiti mgogoro huo unaoendelea nchini mwake, Maduro alizindua taratibu mpya katika tume ya uchaguzi za kuchagua kitengo kinachojitegemea kilichopewa kazi ya kuandika rasimu ya katiba mpya.

Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Reuters/M. Bello

Kiongozi huyo amesema katika televisheni kuwa hio ndiyo njia ya kupatikana amani na maridhiano nchini Venezuela.

"Raia wa Venezuela wanaweza wenyewe kuamua kama wanataka vurugu za magaidi au wanataka amani na ustawi. Venezuela, uamuzi upo mikononi mwenu. Katika wiki chache zijazo, tutakuwa na uchaguzi. Mlitaka uchaguzi, basi mtapata uchaguzi! Mlitaka kupiga kura, basi tutapiga kura! Mlitaka mazungumzo, basi hiki hapa kitengo kinachojitegemea," amesema Rais Nicolas Maduro.

Wapinzani wake wa siasa za wastani za mrengo wa kulia pamoja na mataifa ya kimataifa, wanasema ni hatua ya kujaribu kukwepa chaguzi za mitaa za mwaka huu pamoja na uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwaka 2018.

Idadi ya hivi karibuni iliyotolewa na waendesha mashtaka inasema zaidi ya watu 35 wameuawa ndani ya mwezi mmoja wa maandamano ya kumpinga Maduro, ambaye wapinzani wanamlaumu kwa uchumi wa Venezuela ulioporomoka.

Nchi nane za Amerika Kusini zimezishutumu mamlaka za Venezuela kwa utumiaji wa nguvu dhidi ya raia wake wanaoandamana, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Mexico.

Mataifa hayo manane- Argentina, Brazil, Colombia, Costa Rica, Guatemala, Honduras, Mexico na Paraguay- yamelaani ongezeko la fujo katika taifa hilo linalozalisha mafuta, na kuitaka serikali ya Venezuela kuheshimu haki za binaadamau.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre/dpae

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW