1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi waliokatiza masomo waruhusiwa kurudi shule

25 Novemba 2021

Hatua ya serikali ya Tanzania kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo ikiwamo waliopata mimba kurejea masomoni, inatajwa na kama mwendelezo wa kufumua sera na matamko yaliyosimikwa na hayati John Magufuli.

Symbolbild | Coronavirus & Schwangerschaft | Mundschutz
Picha: picture-alliance/dpa/Pixsell/D. Stanin

Huyu ni Hayati Rais John Magufuli akiweka msimamo wake kuhusu wanafunzi wanaopata mimba kuendelea na masomo. Lakini utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan unaendelea kubadili mkondo kwa kuziweka kando sera zilizokuwa zikihimizwa na mtangulizi wake ingawa  mwenyewe amewahi kusema kuwa yeye na Rais Magufuli ni kitu kimoja. Soma Wajawazito kurejea shuleni Tanzania

Wakati huu baadhi ya mambo ambayo Rais Magufuli aliyapinga waziwazi kutoyatekeleza, yameanza kupewa kipaumbele ikiwamo hatua ya jana ya kuwarejesha wanafunzi waliokatiza masomo kurejea shuleni kuendelea masomoni.

 Zaidi ya watoto 120,000 wamekuwa wakikatiza masomo kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kupata ujauzito. Hatua ya Rais Magufuli kuzuia wanafunzi hao kutorejea shuleni ilipata ukosoaji mkubwa ikiwamo taasisi za kimataifa zilizoona hatua hiyo kama kubinya haki za binadamu.

soma Vifo kwa wajawazito ni changamoto Tanzania

Ingawa aliungwa mkono na wengi ndani ya serikali yake ikiwamo wabunge wa chama tawala, vyama vya upinzani viliendelea kupaza sauti kupinga sera hiyo.

Utawala wa awamu ya sita, unaonekana kujipambanua upya na wachambuzi wa mambo wanasema huenda umehisi namna unavyopaswa kukaribisha mageuzi ili kurejesha matumaini ya ndani na katika jumuiya ya kimataifa pia.

Wachambuzi wanasema?

Picha: Imago Images/fStop Images

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Mohammed Issa anasema pengine lile linalofanywa na utawala wa Rais Samia likawa siyo geni sana katika uso wa siasa za dunia na hasa pale utawala unaoingia madarakani unapoona kuwepo haja ya kufanya hivyo.

"Ni tofauti na nchi za wenzetu suala la maslahi ya kitaifa limewekwa katika katiba kwa hiyo chochote utakachokifanya lazima kiweze kuendana na maslahi ya kitaifa yaliyo kwenye katiba.  Kwa hiyo mabadiliko yanayoendelea kufanyika na rais Samia Suluhu Hassan katika nchi yanaangaliwa kwa mtazamo huo wala sio kwamba itakuakuwa ni mtazamo hasi kwamba anapingana na utawala wa aliyemtangulia alipokuwa makamu wa raisi." amesema Mohammed Issa.

soma  Msaada kwa wajawazito wanaokatisha masomo

Rais Samia amejitofautisha na mtangulizi wake kwa mambo yanayohesabika ikiwamo namna alivyolishughulia janga la maambukizi ya virusi vya corona, janga ambalo wakati wa utawala uliopita lilikuwa likishughulikiwa kwa  namna tofauti. 

Mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa ya Bagamoyo uliofutiliwa mbali na Rais Magufuli, sasa unafufuliwa upya, na tayari serikali ya awamu ya sita iko mboni kuanza majadiliano upya na wawekezaji wake ambao ni serikali ya Uchina.

 

George Njogopa, Dw Kiswahili

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW