1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi wawili Hong Kong waambukizwa kirusi kipya

Sylvia Mwehozi
23 Desemba 2020

Idara ya afya mjini Hong Kong imesema wanafunzi wawili waliowasili kutoka Uingereza wameambukizwa aina mpya ya kirusi cha corona kinachosambaa kwa kasi nchini Uingereza

Hongkong | Flugzeug British Airways, Passagiere
Picha: May James/Zuma/picture alliance

Mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza wa Hong Kong, Dokta Chuang Shuk-kwan amesema sampuli za virusi kutoka kwa wanafunzi wawili waliorejea katika jiji hilo mwezi Desemba, zinashabiiana na aina mpya ya virusi vya corona vilivyozuka huko Uingereza, lakini uchambuzi zaidi utafanywa ili kuthibitisha sampuli.

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam, katika mkutano tofauti na waandishi wa habari siku ya Jumatano, amesema serikali imefanikiwa kupata dozi milioni 7.5 kutoka kampuni ya Oxford ya AstraZenaca na wanatafuta chanzo kingine ili kuweza kujipatia chanjo ya kutosha kwa ajili ya wakazi milioni saba na nusu. Mji huo tayari umenunua dozi za chanjo kutoka kampuni za kichina za Sinovac Biotech na Fosun Pharma-Biontech.

Kiongozi mkuu wa Hong Kong Carrie LamPicha: Lam Yik/Reuters

Nchini Ufaransa afya ya Rais Emmanuel Macron inaendelea kuimarika baada ya kuambukizwa virusi vya corona mnamo Desemba 17. Macron ambaye alijiweka karantini ameendelea kuendesha mikutano kwa njia ya vidio. Mamlaka za Ufaransa zina hofu kwamba msimu wa sikukuu unaweza kuchangia kuongezeka kwa maambukizi, baada ya idadi ya vifo kufikia zaidi ya 60,000 wiki iliyopita. Ufaransa itaanza kutoa chanjo ya corona siku ya Jumapili.

Wakati huo huo, Ufaransa na Uingereza zimefungua tena mipaka yake baada ya saa 48 za marufuku kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha corona. Lakini Uingereza imeonya kwamba zoezi hilo litachukua muda kwa maelfu ya malori yaliyokuwa yamezuiliwa katika bandari ya Dover kuweza kupita.

Nayo kampuni ya Pfizer imesema itaongeza idadi ya dozi milioni 100 za chanjo ya COVID-19 kwa Marekani kufikia mwezi Julai mwakani. Makubaliano ya Jumatano, yanafanya idadi ya dozi iliyonunuliwa na Marekani kufikia milioni 200. Serikali ya Marekani tayari ilikuwa na makubaliano ya dozi milioni 100 na kampuni hiyo ya Pfizer ambayo imeanza kutolewa kote nchini baada ya kupewa idhini ya utoaji chanjo wa dharura mapema mwezi huu.

Misri imefuta maadhimisho ya mwaka mpya ili kupunguza ongezeko la maambukizi ya corona. Waziri Mkuu Mostafa Madbouli amesema hakutokuwa na sherehe za mwaka mpya au mikusanyiko yoyote kama sehemu ya hatua za tahadhari za kukabiliana na maambukizi.