1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi wengine 73 watekwa nyara nchini Nigeria

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
2 Septemba 2021

Polisi nchini Nigeria imetangaza wanafunzi wapato 73 wametekwa nyara na watu waliokuwa na silaha Kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Haya ni mashambulio mapya.

Nigeria Gedenken Entführung 200 Chibok Schülerinnen
Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP

Washambuliaji hao waliivamia shule ya sekondari ya serikali iliyopo katika kijiji cha Kaya, kwenye jimbo la Zamfara na kulingana na msemaji wa polisi Mohammed Shehu, operesheni ya kuwaokoa wanafunzi hao bado inaendelea.

Ibrahim Dosara, kamishna wa habari wa jimbo la Zamfara ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba serikali ya jimbo hilo imeamuru shule zote kufungwa ili kuzuia mashambulio zaidi. Polisi nao wamasema wameongeza doria katika kijiji cha Kaya ili kuzuia mashambulio zaidi dhidi ya jamii.

Shule zimefungwa kwa kuhofia mashambulio na watoto kutekwa nyaraPicha: AFP

Zamfara ni miongoni mwa majimbo manne ya kaskazini magharibi mwa Nigeria ambayo yamechukua hatua madhubuti kudhibiti mgogoro wa usalama. Kwa mfano wamepiga marufuku uuzaji wa mafuta kwenye vidumu na usafirishaji wa kuni kwa malori yote haya ni kwa matumaini ya kupangua mipango ya magenge yanayosafiri na kuweka kambi katika misitu.

Soma zaidi:Wabeba silaha waua 3, wawateka 20 chuoni Nigeria

Hadi kufikia sasa zaidi ya wanafunzi 1,000 wametekwa nyara kutoka kwenye shule za eneo hilo la kaskazini magharibi mwa Nigeria tangu mwezi Desemba mwaka jana. Makundi ya watu wenye silaha wanatumia mbinu zilizotumiwa na waasi wenye itikadi kali za kidini huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Kila wakati unapofanyika utekaji nyara makundi hayo ya wahalifu wenye silaha hudai malipo ya fidia kutoka kwa wazazi na jamaa za wanafunzi hao. Japo kuwa wanafunzi wengi wamebahatika kuachiliwa huru kutoka kwenye mikono ya wahalifu hao, wengine wao wamekufa au wameuawa na magenge katili ya watekaji nyara.

Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: Getty Images/AFP/P.U. Ekpei

Watoto wapatao 90 waliachiwa huru mnamo siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada ya kutekwa nyara na kuzuiwa kwa muda wa miezi mitatu. Mamlaka ilitangaza siku hiyo hiyo kwamba kundi la pili la wanafunzi 15 pia waliachiliwa kutoka mikononi mwa watekaji. Wasichana kwa wavulana walioachiwa waliwasili katika mji wa Minna Ijumaa asubuhi na walikaribishwa na ndugu na jamaa zao kwa furaha kubwa. Maafisa wa serikali pia walikuwa miongoni mwa watu waliowapokea wanafunzi hao.

Vyanzo:/RTRE/AP