1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Wanaharakati: ICC imchunguze Bolsonaro

Angela Mdungu
12 Oktoba 2021

Kundi la wanaharakati wa mazingira, limeitaka mahakama ya ICC ianzishe uchunguzi wa uhalifu dhidi ya ubinaadamu unaodaiwa kufanywa na utawala wa Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro katika sera zake juu ya msitu wa Amazon

Waldbrände im Amazonas Brasilien
Picha: Carl de Souza/AFP/ Getty Images

Kundi hilo la wanaharakati wa mabadiliko ya tabia nchi linaloundwa na wanasheria linaloitwa AllRise liliwasilisha nyaraka kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu  ya ICC, likidai kwamba utawala wa Jair Bolsonaro unahusika na mashambulizi katika msitu wa Amazon, watu wanaoutegemea na wanaoulinda. Wanasheria hao wamesema, matokeo ya mashambulizi hayo yana athari kubwa kwa watu wote duniani.

Tangu alipoingia madarakani, Bolsonaro amekuwa akihimiza kufanyika kwa shughuli za maendeleo kwenye msitu huo na kupuuza malalamiko kutoka pande zote ulimwenguni kuhusu uharibifu ambao unarudisha nyuma kilimo cha biashara nchini Brazil.  Utawala wake pia umedhoofisha mamlaka za mazingira na kuunga mkono hatua za kisheria zinazolenga katika kulinda ardhi huku zikiwapa nguvu wavamizi wa ardhi. 

Uhalifu dhidi ya mazingira ni uhalifu dhidi ya binadamu

Akizungumzia shauri hilo, mwanzilishi wa kundi la wanasheria watetezi wa mazingira la AllRise, Johannes Wesemann amesema uhalifu dhidi ya mazingira ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu na kwamba Rais Bolsonaro anachochea uharibifu mkubwa wa Amazon akiona na kufahamu fika matokeo ya kufanya hivyo. Wesseman amesema mahakama ya ICC ina wajibu wa wazi wa kuchunguza uhalifu wa mazingira kwa uzito wa kimataifa.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wapinzani wa kiongozi huyo wa Brazili kuitaka mahakama hiyo kuingilia kati. Miaka miwili iliyopita, kundi la wanasheria wa Brazil na mawaziri wa zamani waliiomba mahakama hiyo imchunguze Bolsonaro kwa tuhuma za kuchochea mauaji ya halaiki ya wakaazi asilia na kwa kushindwa kulinda misitu na ardhi wanayoishi.

Rais wa Brazil, Jair BolsonaroPicha: Mateus Bonomi/AA/picture alliance

Kumekuwa na ongezeko la wanaharakati kutaka mashtaka ya uhalifu dhidi ya mazingira yawe sehemu ya msingi ya madhumuni ya mahakama hiyo. Mnamo mwezi Juni jopo la wanasheria wa kimataifa lilichapisha pendekezo la maana ya uhalifu wa mazingira ikisema kuwa ni wakati wa kupanua zaidi msingi wa mkataba wa mahakama hiyo ili ijumuishe "Ulinzi dhidi ya madhara kwa mazingira, ambayo tayari yametambuliwa kuwa suala la kimataifa."

Kabla ya Bolsonaro kuingia madarakani mwaka 2019, msitu wa Amazon haukuwahi kuripoti hata mwaka mmoja wenye ukataji miti katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 10,000 kwa zaidi ya miaka kumi. Kati ya mwaka 2009 na 2018  wastani wa ukataji miti ka mwaka ulikuwa kilomita za mraba 6,500 ikilinganishwa na wastani wa kilomita za mraba 10,500 za kipindi cha utawala wa Bolsonaro

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW