1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati Kenya wataka kushirikishwa wazee kwenye jamii

28 Septemba 2018

Mashirika na makundi yanayowahudumia wazee nchini Kenya yanataka mataifa barani Afrika kuzingatia kwa makini haki za wazee miongoni mwa raia wao, kwani hawa ni watu waliotumia umri wao wote kuzijenga jamii na nchi zao.

Kenia Joyce Gichuna aus Nairobi
Picha: DW/R. Kyama

Katika mahojiano na DW, wahudumu mbali mbali wamesikitikia hali mbaya iliyopo na pia mipango dhaifu katika nchi nyingi barani humu pasipokuwa na mwelekeo maalum wa kuwatunza na kuwalinda watu wa umri mkubwa. 

Joyce Gichuna ni mama mkongwe mwenye umri wa miaka 78 na mkazi wa mtaa wa Kahawa West jijini Nairobi. Anasema masaibu chungu nzima yanayowaandama wazee waishio mjini, kama vile ukosefu wa chakula na malazi bora.

Ni kutokana na hilo ambapo wahudumu na mashirika ya kutetea haki za wakongwe nchini wanaiomba jamii ya kitamaifa kuzingatia kwa makini sera zinazowalenga wazee katika jamii ili kuwawezesha kuishi maisha bora na salama. 

Bado Tupo: Heshima kwa Wazee

01:01

This browser does not support the video element.

Elijah Mwega, mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali nchini Kenya linalowasaidia wakongwe, anataka viongozi kutoka nchi za Umoja wa Afrika kufahamu na kuheshimu nafasi ya wazee kwenye bara hilo lenye vijana wengi zaidi kuliko jengine lolote duniani.

Kulingana na Mwega, shirika lake la KARIKA linaendesha kituo maalum cha kuwahudumia wazee katika mtaa wa Dagoretti South jijini Nairobi. Kwa sasa, kituo hicho kinawahudumia wakongwe wapatao 300 kutoka mitaa ya mabanda yenye kuzunguka maeneo hayo. 

Isitoshe, kituo hicho pia huwasaidia akina mama wakongwe walio na jukumu la kuwalea watoto walioachwa mayatima baada ya wazazi wao kufariki kutokana na maambukizi ya virusi vinavyosababisha maradhi ya Ukimwi. 

Oktoba Mosi huadhimishwa duniani kote ili kukumbushana umuhimu wa kuupatia umma wa watu wakongwe hali njema ya afya, raha, ustawi na heshima, mambo ambayo yameonekana kukosekana katika miaka ya karibuni. 

Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef