Wanaharakati Kenya wataka Samia awajibishwe
31 Oktoba 2025
Wanaharakati hao wameutolea mwito Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki kushinikiza Rais Samia Suluhu awajibishwe kwa kile wamekitaja kuwa kuzuwiya maandamano ya amani.
Matamshi ya wanaharakati hao wameyatoa baada ya kuweko ripoti kwamba maandamano yanayoigubika hivi sasa Tanzania yamesababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi wamejeruhiwa.
Matukio ya aina hiyo ni jambo la nadra katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ambalo kwa miongo mingi limepewa sifa ya kisiwa cha amani barani Afrika. Aidha wanaharakati hao wameilaani serikali ya Tanzania kwa kutumia nguvu kupita kiasidhidi ya waandamanaji, waliokuwa wakitekeleza haki yao ya katiba. Hussein Khalid ni mwanaharakati wa shirika la Vocal Africa.
"Tunataka serikali ya Tanzania ikome mara moja kutumia vikosi vya usalama, kunyamazisha, kukandamiza na kuwaua watanzania, tunasema kwamba lazima kuwe na uchunguzi wa wazi kwa yale maovu yaliyotendwa, mauaji na mengineyo.”
Maandamano yalizuka katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine wakati wa kupiga kura siku ya Jumatano, waandamanaji wanasema wanaupinga uchaguzi huo mkuu wakilalamika haukuandaliwa kwa misingi ya haki kufuatia kutokuwepo kwa wagombea wa urais wa vyama vikuu viwili vya upinzani. Rais Samia Suluhu Hassan anayewania kwa mara ya kwnaza chini ya chama tawala, CCM alikuwa anachuana na wagombea wengine 16 wa vyama vidogo.
Tanzania ipo katika mkwamo wa kidemkorasia
Kutokana na maandamano hayo, polisi ilitangaza amri ya kutotoka nje usiku katika jiji la Dar es Salaam, lenye zaidi ya wakazi milioni saba, baada ya ofisi za serikali na majengo mengine kuchomwa moto. Mashirika hayo ya binadamu sasa yanaiomba Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kumwajibisha Rais Samia Suluhu kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Martha Karua ni kiongozi wa chama cha People Liberation Party.
"Ni wakati wa Umoja wa Afrika, kuwahudumia watu wa Afrika, kukoma kuwa kilabu cha viongozi wanaokatalia madaraka na kuelekeza nguvu zake kuwasaidia watu wa mataifa ya bara la Afrika.”
Wanaharakati hao wamesema Tanzania inashuhudia mwamko wa kidemokrasia na vijana ndio wanaolengwa.
"Tunataka serikali ya Tanzania irudishe mtandao nchi nzima, kila Mtanzania ana haki ya kujieleza, kila mtanzania ana haki ya kupata habari, kwa hivyo tunataka haraka iwezekanavyo,” aliongeza kusema Hussein Khalid.
Wakati huohuo, Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Kenya, Dkt. Raymond Omollo, amewataka Wakenya kuzingatia sheria, kufuatia taarifa za baadhi yavijana wa Kenya kukusanyika kwenye mpaka na Tanzania wa Namanga kuonesha mshikamano na wenzao wa nchi hiyo jirani. Dkt. Omollo alisema Kenya ina sheria na kanuni za wazi zinazoongoza maandamano ya umma na akatoa wito wa utulivu huku vyombo vya usalama vikiendelea kufuatilia hali katika mpaka huo.