1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati machachari Hong Kong wafungwa

2 Desemba 2020

Mkosoaji mkubwa katika jiji la Hong Kong Joshua Wong pamoja na wanaharakati wenzake wawili wamehukumiwa kifungo kwa madai ya kushiriki maandamano makubwa ya kudai demokrasia yaliyohanikiza mwaka uliopita.

Hongkong Aktivisten Agnes Chow, Ivan Lam and Joshua Wong vor Gericht
Picha: Peter Parks/AFP/Getty Images

Mkosoaji mkubwa katika jiji la Hong Kong Joshua Wong pamoja na wanaharakati wenzake wawili wamehukumiwa kifungo kwa madai ya kushiriki maandamano makubwa ya kudai demokrasia yaliyohanikiza mwaka uliopita kwenye jiji hilo kitovu cha biashara ulimwenguni katika wakati ambapo hatua kali kuelekea kwa wakosoaji dhidi ya Beijing zikizidi kuchukua mkondo wake.

Wong mwenye miaka 24, alihukumiwa pamoja na wanaharakati wenzake wa karibu wawili Ivan Lam na Agnes Chow kuhusiana na madai hayo ya kushiriki maandamano nje ya makao makuu ya polisi.

"Pamoja na kwamba siku zijazo zitakuwa ngumu, lakini tutavumilia" alisema Wong kwa sauti ya juu wakati akiondolewa mahakamani tayari kuanza kutumikia kifungo gerezani.Hong Kong

Wanaharakati hao watatu, ambao ni miongoni mwa wanaonakena kuwa mwiba mchungu kwa serikali ya Beijing, walikiri baadhi ya mashitaka dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuchochea mkusanyiko batili.

Kulingana na hakimu Wong Sze-lai, hukumu ya haraka ya kifungo ndio lilikuwa chaguo sahihi zaidi. Chow ambaye alimwaga machozi wakati hukumu hiyo ikisomwa, alihukumiwa miezi 10 jela, huku mwenzake Lam akihukumiwa miezi saba.

Chow(kushoto) alianza harakati tangu akiwa mdogo za kushinikiza demokrasia na uhuru wa Hong KongPicha: picture-alliance/NurPhoto

Hong Kong iligubikwa na miezi saba ya maandamano makubwa kabisa yaliyoambatana na machafuko wakati mamilioni walipoingia mitaani.

Licha ya umri mdogo wa wanaharakati hao, Wong na Lam tayari wamewahi kutumikia kifungo jela kwa kuongoza maandamano ya demokrasia.

Wong na wenzake wanasema harakati zitaendelea hata baada ya hatua kali.

Kiongozi wa waandamanaji wanafunzi Nathan Law ambaye pia aliwahi kuonja joto la kifungo gerezani Hong Kong na baadaye kukimbilia Uingereza amesema kuwafunga gerezani wale wanaoshinikiza demokrasia hakutazimisha ushawishi wao kwenye harakati hizo. Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, haamini kama hatua hiyo itawarudisha nyuma.

Wong na Lam walijiunga na harakati za kudai demokrasia tangu wakiwa na umri mdogo. Kwa pamoja waliandaa maandamano yaliyofanikiwa pakubwa mnamo mwaka 2012 dhidi ya mipango ya ya kuugeuza mfumo wa elimu kuwa wa "kizalendo" zaidi, pamoja na kushiriki maandamano mengine ya kudai haki na demokrasia.

Jeshi la polisi Hong Kong latishia kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji

00:53

This browser does not support the video element.

Joshua Wong hata hivyo ameapa kuendeleza kampeni ya kudai demokrasia licha ya kifungo hicho. Ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba huo sio mwisho wa harakati. Ujumbe wake ulisambazwa na wanasheria wake baada ya hukumu hiyo. Aliongeza kuwa, bado kuna mapambano mengine makali huko siku za usoni na kwamba kwa sasa wanaungana na wanaharakati wenzao walioko jela, ambao hawalengwi sana, lakini wenye ushawishi mkubwa katika mapambano ya kusaka demokrasia na uhuru wa Hong Kong, ulisema ujumbe wake huo.

Uingereza umeiomba Hong Kong na Beijing kuachana na kampeni za kuudidimiza upinzani kufuatia hukumu hiyo. Waziri wa mambo ya kigeni Dominic Raab amesema hukumu zinatakiwa kuwa za haki na zisizo za upendeleo, na uhuru na haki za watu wa Hong Kong ni lazima viheshimiwe.

Mashirika: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW