Wanaharakati Myanmar waitisha kampeni mpya dhidi ya jeshi
26 Aprili 2021Maandamano ya hapa na pale yalifayika katika miji mikubwa nchini Myanmar jana Jumapili, siku moja baada ya Jenerali mwandamizi Min Aung Hlaing kufikia makubaliano ya kukomesha mzozo, wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa mataifa ya jumuiya ya ushirikiano wa kusini mashariki mwa Asia, ASEAN, uliofanyika nchini Indonesia wiki iliyopita.
Utawala huo wa kijeshi haukusalimu kwa miito ya kuwaachia wafungwa wa kisiasa, akiwemo kiongozi wa serikali ya kiraia Aung San Suu Kyi, na makubaliano hayo ya ASEAN yalikosa ratiba yoyote ya kukomesha mzozo.
Soma pia: Amnesty yaorodhesha ukatili dhidi ya waandamanaji Myanmar
Siku ya Jumatatu utawala huo wa kijeshi uliahirisha tena kesi ya mahakamani dhidi ya Aung San Suu Kyi, wakati mawakili wakipambana kupata ruhusa ya kumtembelea, wiki 12 tangu alipokamatwa.
''Kesi iliahirishwa hadi Mei 10 kwa sababu ya suala moja tu: kuhusu jibu la polisi juu ya iwapo kuwekwe utaratibu wa mkutano kati ya washtakiwa na mawakili,'' alisema mmoja wa mawakili hao Khin Maung Zaw.
Mawakili hao waliomba mkutano kama huo mapema, lakini mahakama ilikuwa haijawakubalia ombi lao.
Urusi yasema inapendelea suluhisho la ndani
Suu Kyi anakabiliwa na jumla ya mshtaka sita, yakiwemo ukiukaji wa sheria za biashara ya nje, kuhusiana na vifaa vya mawasiliano ya redio za mkononi vilivyokutikana nyumbani kwake na kukiuka vikwazo vya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.
Mashtaka mazito zaidi mpaka sasa ni kuhusu uchochezi wa uasi.
Soma pia: Hali yazidi kutisha Myanmar
Kundi la wanaharakati wa ufautialiaji linasema watu 751 wameuawa na vikosi vya usalama katika matumizi ya nguvu ya majenerali dhidi ya maandamano endelevu yalioanza tangu mapinduzi ya Februari Mosi.
Kampeni ya uasi wa umma imezorotesha uchumi, na mashirika ya kimataifa ya misaada yameonya juu ya uwezekano wa kuzuka njaa.
Wanaharakati wa demokrasia wametoa wito wa kuimarisha juhudi zao siku ya Jumatatu, kwa kukataa kulipa bili za umeme na mikopo ya kilimo, na kwa watoto kuacha kwenda shuleni.
Ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema leo kuwa inapendelea suluhisho la ndani kwa mzozo wa Myanmar, huku ikisema pia kwamba Urusi inalaani vikali vitendo vyovyote vinavyosababisha vifo vya raia.
Mapema mwezi huu, Urusi ilionya kwamba vikwazo dhidi ya watawala wa kijeshi nchini Myanmar vinaweza kuisukuma nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Chanzo: Mashirika