Wanaharakati Uganda wapinga washukiwa kuuawa
23 Novemba 2021Wanapendendekeza serikali ifanye mazungumzo na kundi la waasi wa ADF ambalo linadaiwa kuleta hali ya sintofahamu si tu katika nchi jirani ya Congo lakini pia nchini Uganda wanakodaiwa kuhusika katika kuripua mabomu.
Katika kipindi cha miezi minne sasa watu wanaoshukiwa kuhusika katika ugaidi wameuawa na vyombo vya usalama nchini Uganda huku zaidi ya mia wakikamatwa bila kufikishwa mahakamani. Watu hao wanadaiwa kuwa wa kundi la Allied Democratic Front ADF , kundi la waasi kutoka Uganda ambalo hudaiwa kuendesha harakati zao kutoka ngome zao Mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mauaji ya hivi majuzi ya sheikh mmoja ambaye familia yake wanasisitiza aliuawa akiwa amefungwa pingu baada ya kukamatwa yameibua tena mjadala kwa nini washukiwa wauawe badala ya kufikishwa mahakamani. Rais Yoweri Museveni anasisitiza kuwa kile wasichafahamu wananchi, watu hao ni hatari na hujaribu kukabiliana na maafisa wa vyombo vya usalama pale wanapokamatwa na kwa hiyo kuwaua ndiyo hatua ya pekee ya maafisa hao kuhakikisha usalama wao.
Lakini ufafanuzi wa rais Museveni umepingwa vikali na watetezi wa haki za binadamu , viongozi wa kidini na wanasiasa wa upinzani. Wanahoji kwa nini mshukiwa auawe bila kupitishwa katika mchakato wa kisheria na kwa hiyo ni rahisi mtu asiye na hatia kuua.
Tangu mapema miaka ya 2000, kundi la ADF limehusishwa na mashambulio kadhaa na mauaji ya raia hasa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Juhudi za kukomesha harakati za nchi hiyo zimelezewa kuhitaji ushirikiano wa Uganda na serikali ya Congo. Lakini haijafahamika kwa nini suala hilo limechelewa kushughulikiwa na pande zote mbili licha ya raia wa Congo kutoa kilio cha mashambulizi ya mara kwa mara. Sasa baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani nchini Uganda wanapendekeza serikali izingatie kuanzisha mazungumzo ya amani na waasi wa ADF.
Chama cha Wanasheria wa Kiislamu nchini Uganda nacho kimetoa mwito kwa serikali kukomesha mauaji ya washukiwa wa ugaidi . Kina mtazamo kuwa mwenendo wa kuwaua washukiwa utazidi kuleta mashaka kama kweli vyombo vya usalama vina nia ya kukomesha hali ya isntofahamu ya mashambulizi ya mabomu ikiwa hawana nia kufanya uchunguzi.Lubega Emmanuel DW Kampala