1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati vijana waandamana katika mkutano wa COP26

Sylvia Mwehozi
5 Novemba 2021

Mamia ya wanaharakati vijana wa mazingira wamekusanyika mjini Glasgow kupinga kile walichokitaja kama hatari ya kukosekana kwa hatua kutoka kwa viongozi wa ulimwengu katika mkutano wa mazingira wa COP26. 

Cop26 - Glasgow
Picha: Andrew Milligan/empics/picture alliance

Siku mbili za maandamano yatakayofanyika Ijumaa na Jumamosi, zimepangwa kuelezea kasi ndogo ya upunguzaji gesi chafu na dharura ya hali ya hewa ambayo tayari imeenea katika nchi zote ulimwenguni. Umati mkubwa ulioandaliwa na vuguvugu la maandamano ya Ijumaa kwa ajili ya Mustakabali, ulianza maandamano yake katikati mwa Glasgow huku wanaharakati wakubwa kama vile Greta Thunberg na Vanessa Nakate wakitarajiwa kuhudhuria. Brianna Fruen ni mwandamanaji kijana wa New Zealand.

"Nimepitia vimbunga vitatu vikubwa. Nimeona mafuriko yakiingia nyumbani kwetu. Nimesema asubuhi ya leo kwamba nakumbuka harufu ya matope, matope yanafika katika magoti yako kwa sababu hiyo ndiyo hali halisi ya mafuriko yanapoingia. Hiyo ndio hali halisi ya maisha ya vijana, vijana wanaoishi ndani ya jamii zinazoathiriwa na hali ya hewa."

Wajumbe kutoka takribani mataifa 200 wako mjini Glasgow kupanga jinsi ya kutekeleza malengo ya mkataba wa Paris ya kuzuia ongezeko la joto ulimwenguni kufikia kati ya nyuzi 1.5 na 2. Mchakato huo unaongozwa na Umoja wa Mataifa unahitaji nchi kujitolea katika kuongeza juhudi za kupunguza gesi chafu na kuzitaka nchi tajiri ambazo kihistoria ndio wachafuzi wakubwa, kuyasaidia mataifa yanayoendelea kufadhili mabadiliko ya nishati na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kinara wa maandamano ya vijana kuhusu mazingira Greta ThunbergPicha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Hapo Alhamis nchi zilitoa ahadi mbili za ziada katika kupunguza matumizi ya nishati ya ardhini. Mataifa 20 yakiwemo wafadhili wakuu Marekani na Canada yaliahidi kukomesha ufadhili wa nje wa nishati hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka ujao. Hata hivyo, makundi ya wanaharakati wa mazingira wamegusia kwamba serikali hususan mataifa tajiri ambayo ndio wachafuzi wakubwa yamekuwa na hulka ya kushindwa kutekeleza ahadi zake juu ya mazingira.

Mjumbe wa Marekani kuhusu mazingira John Kerry amesema kwamba kuna uwezekano wa kufikia makubaliano katika mkutano wa COP26 na kumalizia maelezo ya mwisho ya mwongozo wa namna ya kutafsiri mkataba wa Paris wa 2015.

Kerry amesema Marekani inaunga mkono tathmini ya mara kwa mara ya ikiwa nchi zinatimiza malengo ya mkataba huo unaolenga kupunguza utoaji wa gesi chafu.

Wakati huo huo, makampuni makubwa ya usafirishaji leo yamezitaka serikali kuelekeza fedha zaidi katika utafiti na teknolojia safi ambazo zitasaidia viwanda kupunguza uzalishaji wa hewa chafu. Chama cha kimataifa cha wasafirishaji kimesema sekta hiyo haiko katika mkondo wa kutimiza malengo yake ya kupunguza gesi chafu ya ya Kaboni hadi kiwango sifuri kufikia mwaka 2050 kulingana na sera zilizoko. Kwa hivi sasa usafirishaji unachangia karibu asilimia 3 ya hewa chafu ulimwenguni.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW