1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wa Global Sumud Flotilla wailalamikia Israel

6 Oktoba 2025

Wanaharakati wa msafara misaada ya kibinaadamu kwa Gaza, Global Sumud Flotilla, uliovamiwa na kutekwa na jeshi la Israel, wanalalamikia kutendewa vibaya mikononi mwa mamlaka za Israel, huku wengi wakirejeshwa makwao.

Turkiye Istanbul 2025 | wanaharakati wa Global Sumud Flotilla
Baadhi ya wanaharakati wa msafara wa Global Sumud Flotilla waliokuwa wametiwa nguvuni nchini Israel wakipunga mikono baada ya kuwasili mjini Istanbul, Uturuki, siku ya Jumapili (Oktoba 5, 2025).Picha: Muhammed Enes Yildirim/Anadolu/picture alliance

Ndege iliyowabeba wanaharakati 29, ambapo 21 ni raia wa Uhispania, iliruka siku ya Jumapili (Oktoba 5) kutoka uwanja wa ndege wa Tel Aviv na kutuwa kwenye uwanja wa ndege wa Barajas mjini Madrid nyakati za usiku.

Kati yao, alikuwamo meya wa zamani wa mji wa Barcelona, Ada Colau, na mbunge wa Esquerra, Jordi Coronas.

"Tumekutana na hali ngumu sana, tumewekwa kizuizini kinyume na sheria, tumeshambuliwa tukiwa kwenye bahari ya kimataifa. Tuliwekwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali ambako haki zetu hazikuheshimiwa, kulikuwa na udhalilishaji mkubwa. Lakini tunajuwa haya si chochote yanapolinganishwa na yale wanayopitia Wapalestina kila siku na kile kinachotokea Gaza." Alisema Meya Ada Colau mara alipowasili mjini Madrid.

Wanaharakati wengine 28 wa Kihispania waliotiwa nguvuni na jeshi la Israel na ambao waliendelea kubakia jela kwa sababu ya kukataa kusaini hati ya kutambuwa kuwa kuingia kwao nchini humo kulikuwa kinyume na sheria, walikuwa wanatazamiwa kurejeshwa makwao siku ya Jumatatu (Oktoba 6), kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Uhispani, Jose Manuel Albares.

Wanaharakati hao walikuwa bado wanashikilia kwamba safari yao ilikuwa ni kuelekea  Ukanda wa Gaza, ambayo si sehemu ya Israel, licha ya kwamba imezingirwa kijeshi na Israel.

Wanaharakati wa Kiislamu, Kiarabu walikumbana na hali mbaya zaidi

Mwanaharakati mwengine, Marco Tesch, raia wa Uholanzi mwenye asili ya Palestina, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mateso aliyopitia yalikaribia kumtoa roho na kwamba wenye asili ya Kiarabu na Kiislamu walikuwa wanapata tabu zaidi.

Maandamano ya kuwaunga mkono wanaharakati wa msafara wa Global Sumud Flotilla na kuilaani Israel kwa kuwakamata yaliyofanyika mjini Barcelona, Uhispania, siku ya Jumamosi (4 Oktoba 2025).Picha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

"Mimi mwenyewe nina asili ya Kipalestina. Siku ya mwanzo kabisa nilianza kutendewa vibaya. Nilikaribia kukata roho kwa kuwa walinigubika usoni na kunifunga mikono kwa nyuma. Na tulipokuwa jela, maafisa wa Israel walikuwa wakimtesa kila mtu kutoka Tunisia au Malaysia au nchi yoyote ya Kiislamu au ya Kiarabu, na wakaondoka nao, kwa sababu hawana mabalozi wa nchi zao, walikuwa hawapati msaada." Alisema mwanaharakati huyo.

Wanaharakati sita waliowasili nchini Uswisi siku ya Jumapili nao pia walilalamikia mateso na hali mbaya ya kibinaadamu walipokuwa mikononi mwa vyombo vya usalama nchini Israel. 

Raia 19 wa Uswisi, akiwemo meya wa zamani wa mji wa Geneva, Remy Pagani, walikuwamo kwenye msafara huo wa Global Sumud Flotilla uliokuwa unajaribu kuvunja mzingiro wa kijeshi wa Israel na kuwafikia watu wa Gaza kwa misaada ya kibinaadamu.

Miongoni mwa waliotarajiwa kuachiwa siku ya Jumatatu ni mwanaharakati mashuhuri wa Sweden, Greta Thunberg, akiungana na wenzake 70 kutoka mataifa mbalimbali.

Wengi wao walipangiwa kupelekwa kwanza nchini Ugiriki, ambako kisha wangepatiwa usafiri wa kuelekea makwao.

Waliotakiwa kuruka Jumatatu ni raia 28 wa Ufaransa, 27 wa Ugiriki, 15 wa Italia na tisa wa Sweden.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW