Wanaharakati wa Kenya waachiwa huru Uganda
9 Novemba 2025
Wanaharakati wawili raia wa Kenya, Bob Njagi na Nicholas Oyoo, walitoweka Oktoba baada ya kusafiri kwenda taifa jirani la Afrika Mashariki kumuunga mkono kiongozi wa upinzani wa Uganda Bobi Wine, ambaye anakusudia kugombea urais dhidi ya rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni, aliye madarakani kwa muda mrefu, katika uchaguzi mwaka ujao.
Katika taarifa fupi ya pamoja katika mtandao wa kijamii wa X, mashirka vya haki za binadamu Amnesty Kenya, Vocal Africa na Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK) yalisema "yanakaribisha kuachiliwa huru kwa Nicholas Oyoo na Bob Njagi jana usiku huko Busia baada ya siku 38 za kutoweka kwao kulikolazimishwa".
Taarifa hiyo, iliyochapishwa na mkuu wa LSK Faith Odhiambo, haikutoa maelezo zaidi lakini ilisema "wanawezesha uhamisho wao kwenda Nairobi". Taarifa hiyo ilitoa shukrani kwa makundi ya kutetea haki za binadamu, pamoja na wizara za kigeni na raia wanaofanya kazi ambao "walifanya kampeni bila kuchoka kwa wakati huu".
Kaka mkubwa wa Oyoo, Nobert Ochieng, 53, alliiambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba familia yake "ilifurahi" kutokana na habari hiyo. "Ilikuwa faraja kubwa, kwa sababu umekuwa mwezi mgumu na wenye mateso makubwa kwetu," alisema.
Mudavadi athibitisha kuachiwa kwa wanaharakati
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi alithibitisha kwamba wanaharakati hao wawili waliachiliwa Ijumaa jioni baada ya "ushirikiano endelevu wa kidiplomasia".
Mipango ilikuwa ikiendelea ili "kuhakikisha Wakenya hao wawili wanaungana tena salama na familia zao", aliongeza kuandika katika chapisho kwenye mtandao wa X. Wanaharakati hao walitoweka mwezi uliopita, huku polisi wa Uganda wakikana kwamba mwanaharakati yeyote alikuwa kizuizini.
Makundi ya haki za binadamu na familia za wanaume hao nchini Kenya yamesitasita kurejea kwao, yakikata rufaa kwa mahakama ya Uganda na kuiomba serikali kufichua mahali walipo.
Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Kenya VOCAL Africa, Hussein Khalid, alisema mwezi uliopita kwamba mashahidi waliripoti kuwa wanaume hao wawili walichukuliwa na "wanaume waliovaa barakoa, waliovaa sare na wenye silaha, wakidokeza ushahidi thabiti wa kuhusika kwa serikali katika kutoweka kwao.
"Tunashuku kwamba wawili hao wanaweza kuzuiliwa pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa wa Uganda katika vituo vya kijeshi," alisema.
Wakosoaji wengi wa serikali na watu wa upinzani wametekwa nyara katika miaka ya hivi karibuni kote Afrika mashariki, na makundi ya haki za binadamu yanadai mamlaka yanashindwa kuwalinda raia wao na hata kufanya kazi pamoja dhidi ya wanaharakati.
Mwezi Mei, mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire wanasema walitekwa nyara na kuteswa na vikosi vya usalama nchini Tanzania, na hawakupata msaada mkubwa kutoka kwa serikali zao.