1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na Haki

Wanaharakati wataka mauaji ya wanawake yakomeshwe Kenya

Sylvia Mwehozi
6 Septemba 2024

Makundi ya wanawake nchini Kenya yametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mwanariadha Rebecca Cheptegei aliyefariki dunia
Mwanariadha Rebecca Cheptegei aliyefariki dunia Picha: Chai v.d. Laage/IMAGO

Makundi ya wanawake nchini Kenya yametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki baada ya kifo cha mwanariadha mwingine kilichosababishwa na mpenzi wake. Mwanariadha Rebecca Cheptegei alifariki dunia jana, siku nne baada ya mpenzi wake kumwagia petroli na kumchoma nyumbani kwake magharibi mwa Kenya. Mwanariadha huyo ni wa tatu wa kike kuuawa nchini Kenya tangu mwaka 2021.

Mwanzilishi wa shirika la Usikimye linalopambana na ukatili wa kijinsia Njeri Migwi amesema ukatili mwingi wa kijinsia hauchukuliwi kuwa ni uhalifu na hivyo kuitaka serikali kuchukua hatua. Takwimu za idadi ya wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia nchini Kenya zinatofautiana sana, ambazo wanaharakati wanasema hufunika ukubwa halisi wa tatizo

Mwaka 2022, wanawake 725 walikufa nchini Kenya katika mauaji yanayohusiana na ukatili wa kijinsia, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2015. Takwimu hizo zilikusanywa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu.Mwanariadha wa Uganda afariki baada ya mpenzi kumchoma moto

Mauaji ya Cheptegei yanafuatia mauaji ya wanariadha wawili maarufu wa Kenya. Mnamo Oktoba 2021, mwanariadha Mkenya aliyevunja rekodi Agnes Tirop, 25, aliuawa kwa kuchomwa kisu nyumbani kwake huko Iten. Mumewe aliyeachana naye yuko mahakamani kuhusu mauaji yake na amekana mashtaka.  Mnamo Aprili 2022, mwanariadha mwingine mzaliwa wa Kenya raia wa Bahrain Damaris Mutua pia alipatikana amekufa huko Iten katika tukio linaloshukiwa kuwa la unyanyasaji wa nyumbani.