Wanajeshi 1,000 wa Afrika wawasili Mali
22 Januari 2013Kulingana na msemaji wa jeshi la Ufaransa, Kanali Thierry Burkhard, wanajeshi 1,000 ambao wameshawasili Mali ni kutoka Nigeria, Togo, Benin, Niger na Chad. Ufaransa yenyewe ina zaidi ya wanajeshi 2,000 wa ardhini nchini Mali, na imepokea msaada wa vifaa vya kijeshi kutoka kwa washirika wake wa kimataifa kutoka magharibi na pia taarifa za kijasusi kutoka Marekani.
Hata hivyo Ufaransa ina matumaini kuwa wanajeshi wa eneo la magharibi mwa Afrika watakuwa katika msitari wa mbele pamoja na wenzao wa jeshi la Mali ambao ni mkoloni wa zamani wa Ufaransa, katika kuiokomboa nchi hiyo kutoka mikononi mwa waasi.
Vikosi vya nchi hizo mbili, Urafansa na Mali, jana viliingia katika miji mikubwa ya mali ya Diabaly na Doutenza, miji ambayo ilikuwa chini ya udhibiti wa waasi kwa wiki kadhaa. Magari ya kijeshi karibia 30 yaliyokuwa na wanajeshi 200 wa nchi hizo mbili yalifululiza katika miji hiyo iliyo kilomita 350 kutoka mji mkuu wa Mali, Bamako.
Kulingana na wakaazi waliobakia katika miji hiyo waasi walitoroka pindi vikosi hivyo vilipokuwa vikiwasili. Wakaazi wengi wa miji hiyo wametoroka kwa hofu ya mapigano. Wachache waliobakia wanahitaji msaada wa kibinaadamu kama chakula na mahitaji mengine muhimu.
Gaoussou Kone, mwenye umri wa miaka 34, na ambaye ni mkaazi wa mji wa Diabaly, amesema wanashukuru kuwepo kwa vikosi vya Ufaransa kwa kuwa iwapo wasingeingilia kati, waasi wangefanikiwa sio tu kuuteka mji wa Diabaly bali Mali nzima.
Mataifa jirani kutarajiwa kutoa msaada Mali
Mataifa jirani na Mali yanatarajiwa kutuma wanajeshi takriban 3,000 lakini namna vikosi hivyo vitakavyofanya kazi na ufadhili wake pia ni jambo ambalo limechelewesha nchi kadhaa kutuma wanajeshi wake.
Ufaransa iliingia Mali Januari 11 mwaka huu kupambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Vikosi hivyo vikishirikiana na vile vya serikali ya Mali kwa sasa vimefanikiwa kuikomboa miji kadhaa iliyokuwa inadhibitiwa na waasi.
Huku hayo yakiarifiwa rais wa Niger, Mahamadou Issoufou, amekitembelea kikosi cha wanajeshi 500 katika kambi ya kijeshi kaskazini mwa mji mkuu, Niamey wanaosubiri amri ya kujiunga na kikosi cha Afrika kinachoongozwa na Nigeria kuingia Mali kupambana na waasi wa kiislamu.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP
Mhariri: Josephat Charo