1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 15 wa Kijerumani wajeruhiwa Mali

25 Juni 2021

Mali inakabiliana na uasi wa makundi ya itikadi kali yanayoendesha uasi mkubwa hasa katika eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo ya Sahel

Mali | UN Minusma Mission | Soldaten der Bundeswehr
Picha: Alexander Koerner/Getty Images

Wanajeshi 15 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali wamejeruhiwa kufuatia mripuko wa bomu la kutegwa ndani ya gari kaskazini mwa nchi hiyo. Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa na Umoja wa Mataifa likiwa ni shambulio la hivi karibuni kabisa katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita ya Ukanda wa Sahel.

Umoja wa Mataifa umeandika kwenye ukurasa wa Twitta kwamba shughuli ya kuwaondoa wanajeshi waliojeruhiwa inaendelea baada ya shambulio hilo lililotokea kambi ya muda ya jeshi karibu na mji wa Tarkint kaskazini mwa Mali ambako hakuna usalama.

Umoja huo haukutowa maelezo zaidi. Hata hivyo mbunge mmoja katika kamati ya ulinzi ya bunge la Ujerumani ambaye hakutaka kutajwa jina na waandishi habari wa shirika la AFP amesema kwamba wanajeshi wote waliojeruhiwa ni wa kikosi cha Ujerumani na 12 kati yao wako katika hali mbaya.

Picha: Joerg Boethling/imago images

Kiasi wanajeshi 13,000 kutoka nchi mbali mbali wako nchini Mali chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA ambacho kinahusika kusimamia amani katika nchi hiyo ambayo sehemu kubwa ni jangwa.

Mali inapambana kudhibiti uasi wa makundi ya itikadi kali ambao ulizuka mwaka 2012 na ambao umeshasababisha vifo vya maelfu ya wanajeshi na raia.

Licha ya kuwepo maelfu ya wanajeshi wa Ufaransa na kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa mgogoro umefika hadi katikati ya nchi hiyo na kusambaa mpaka katika nchi jirani za Burkina Faso na Niger.

Picha: Getty Images/AFP/A. Risemberg

 Afisa mmoja wa masuala ya usalama aliyekataa kutambulishwa kwa jina lake amewaambia waandishi habari wa AFP kwamba kambi inayoongoza shughuli za jeshi hilo iliyoshambuliwa leo ijumaa ilitengenezwa siku moja kabla baada ya  bomu la ardhini kuharibu gari la Umoja wa Mataifa katika eneo hilo. Wanajeshi walijenga kambi ya muda ili kupata nafasi ya kuondoa gari lililoharibiwa kwa mujibu wa afisa mmoja wa usalama.

Itakumbukwa kwamba siku ya Jumatatu wanajeshi 6 wa Ufaransa na raia wanne walijeruhiwa baada ya gari lililokuwa limetegwa bomu kuripuka karibu na gari la silaha la wanajeshi hao wa Ufaransa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

      

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW